1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Israel yashambulia maeneo ya Syria

Sekione Kitojo
9 Januari 2018

Israel imeshambulia  maeneo ndani  ya  ardhi  ya Syria mara tatu  mapema leo Jumanne kwa  ndege  za  kivita pamoja  na  makombora , limesema  jeshi  la  Syria katika taarifa  iliyotangazwa  na  televisheni  ya  taifa.

Israel Kampfjet F-35
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Ndege  za  jeshi la Israel  zimeshambulia  eneo  la Qutayfeh  kaskazini  mashariki  mwa  mji  mkuu  Damascus , na  makombora  yaliangukia  karibu  na  maeneo  ya kijeshi  na  kusababisha  jeshi  la  Syria  kushambulia  kwa kulipiza , na  kuangusha moja  kati  ya  makombora hayo, jeshi  la  Syria  limesema.

Vikosi vya ardhini vya jeshi la Israel katika mashambulizi maeneo ya milima ya GolanPicha: Getty Images/AFP/J. Marey

Israel  pia  ilifanya  mashambulio  ya  makombora  ya ardhini  ndani  ya  Syria  kutoka  katika  eneo  linalokaliwa na  Israel  la  milima  ya  Golan, lakini  jeshi  la  Syria limeyashambulia   makombora  hayo, taarifa  hiyo  ilisema.

Taarifa  ilisema  kwamba  ndege  za  jeshi  la  Israel zilishambulia  tena  kwa  mara ya  mwisho kwa maroketi manne  kutoka  ndani  ya  Israel, na  kwamba mfumo  wa ulinzi  wa  anga  wa  Syria  ulifanikiwa  kuangusha  moja kati ya  makombora  hayo.

Jeshi  la  Syria limesema mfumo wa kulinda  anga umefanikiwa  kuangusha  moja  ya  makombora  hayo na mengine  yaliangukia  katika  moja  kati  ya  maeneo  ya kijeshi  ya  syria, na  kusababisha  uharibifu  wa  mali.

Syria yashambuliwa mara kwa  mara  na  Israel 

Jeshi  la  Israel  limekuwa  likifanya  mashambulizi  mara kwa mara  dhidi  ya  jeshi  la  Syria  na  washirika  wake  wa Lebanon, wa  kundi  la  Washia  la  Hezbollah  tangu mwanzo  wa  mzozo  wa  ndani  wa  Syria  mwaka  2011.

Wapiganaji wa kundi la Hezbollah la LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Central Military Media

Msemaji  wa  jeshi  la  Israel  alikataa  kuelezea  lolote kuhusiana  na  taarifa  iliyotolewa  na  Syria. Licha  ya kuwa  mkuu  wa  jeshi  la  Israel  mwezi  Agosti  mwaka jana  alisema  kwamba  wanajeshi  wake  waliishambulia Syria  karibu  mara  100, sera  za  Israel  kwa  jumla  ni kutothibitisha  ama  kukataa  operesheni  kama  hizo.

Israel  imeapa kuizuwia Iran  kutumia  ardhi  ya  Syria kuweka  vituo vyake  vya  kijeshi  ama  kupitishia  silaha nzito  kwenda  kwa  kundi  la  Hezbollah  nchini  Lebanon, kundi  ambalo  limekuwa likisaidia  Syria  katika  vita  vyake vya  wenyewe  kwa  wenyewe  vya  miaka  sita sasa.

Katika  taarifa  yake  jeshi la  Syria  lilirejea  onyo  lake  la hapo  kabla  la  kulipiza  kisasi  kwa  mashambulizi  hayo ya  anga  na  kurudia  shutuma  zake  za  hapo  kabla kwamba  Israel  inatumia  mashambulizi  hayo kusaidia makundi  ya  wanamgambo  nchini  Syria.

Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Presidency

Israel  ilikamata  kilometa  1,200  za  milima  ya  Golan kutoka  Syria  katika  vita  vya  siku  sita  vya  mwaka  1967 na  baadaye  kulichukua  kabisa  eneo  hilo  katika  hatua ambayo  haijatambuliwa na  jumuiya  ya  kimataifa. Syria na  Israel  zinaendelea  kuwa  katika  hali  ya  kivita, na taifa  hilo  la  Kiyahudi  lilipigana  vita  vikali dhidi  ya Hezbollah  mwaka  2006.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW