Majeshi ya kigeni yashambuliwa Kaskazini mwa Syria
16 Januari 2019Kulingana na shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, takriban watu saba wameuwawa na watu wengine tisa wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Kundi linalojiita dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio hilo. Taarifa za kijeshi na kutoka kwenye baraza la kijeshi la mji wa Manbij unaosimamiwa na wakurdi, imesema mlipuko huo ulitokea karibu na mgahawa ulio karibu na soko kuu la mji huo. Mashambulizi hayo yametokea wakati ambapo majeshi ya Marekani yameanza mchakato wa kuondoka kutoka Syria.
Wakati huo huo mkuu wa jeshi maalumu la Iran la walinzi wa mapinduzi amesema majeshi ya Iran asilani hayataondoka Syria. Mkuu huyo ametoa kauli hiyo leo sambamba na kupinga vitisho vilivyotolewa na Israel.
Shirika la habari la kihafidhina la Fars limemnukulu Meja Jenerali Mohammed Ali Jafar akisema wanajeshi wa Iran washauri na zana zote za kijeshi zinazohitajika kwa ajili ya kuwaimarisha wanajeshi hao zitaendelea kuwapo nchini Syria kwa lengo la kuwasaidia watu wa Syria wanaokandamizwa. Kauli ya Jenerali huyo inazingatiwa kuwa jibu kwa vitisho viliyvotolewa na waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye hapo jana aliiambia Iran iyaondoe majeshi yake kutoka Syria. Nao wapiganaji wa kikurdi wa kikosi cha YPG wamelikataa pendekezo la Marekani juu ya kutenga ukanda wa usalama chini ya usimamizi wa majeshi ya Utruki kaskazini mwa Syria. Na Urusi imesema ni majeshi ya Syria tu yanayopaswa kusimamia ulinzi sehemu hiyo.
Kiongozi mwandamizi wa wapiganaji wa Kikurudi YPG amesema, baada ya kulipinga pendekezo la Marekani, wakurdi hao wako tayari kuyakubali majeshi ya Umoja wa Mataifa yawekwe kwenye sehemu inayowatenganisha wapiganaji wao na majeshi ya Uturuki, ili kuzuia mashambulio ya Uturuki na kwamba wanatarajia kufikia makubaliano na jirani yao Uturuki kuhakikisha utulivu katika eneo la mpakani.
Mapema wiki hii rais wa Uturuki Recp Tayyip Erdogan alisema kuwa majeshi ya nchi yake yatatenga ukanda wa usalama kaskazini mwa Syria baada ya rais Donald Trump kutoa wazo hilo. Rais Erdogan alisema hayo siku moja baada ya mazungumzo yake na rais Trump kwa njia ya simu.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFP/RTRE/AP
Mhariri: Josephat Charo