1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya kigeni yasije! waonya al Shabaab

22 Juni 2009

Hali ni tete Somalia. Kundi la wapiganaji wa al Shabab wametisha kuwashambulia wanajeshi wowote wa kigeni watakaoingia Somalia ili kuisaidia serikali kupambana na uasi. Uongozi wa nchi hiyo umeyatolea wito mataifa jirani

Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Aweys(kushoto) akizungumza na kamishna wa maendeleo wa EU Louis MichelPicha: AP


Kauli hizo zinazoungwa mkono na Umoja wa Afrika. Wakati huohuo, katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, OIC, ameitolea wito jamii ya kimataifa kuingilia kati. Kiasi cha watu 300 wameuawa katika mapigano hayo yaliyodumu kwa kipindi cha majuma sita yaliyopita. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa, wengine 125,000 wameachwa bila makazi.


Kundi la al Shabaab limeonya jana kuwa endapo vikosi vya vya kigeni vitaingia Somalia kuisaidia serikali wapiganaji hao watakuwa hawana budi kuwashambulia. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa kundi la al Shabaab, Sheikh Ali Mohammed Rage, aliyefanya mkutano na waandishi wa habari mjini Mogadishu.

Kauli hizo zimetolewa baada ya spika wa Bunge la Somalia, Sheikh Aden Mohamed Nur Madobe, kuyatolea wito mataifa jirani ya Djibouti, Kenya na Ethiopia kuvipeleka vikosi vyao katika kipindi cha saa 24 kwa minajili ya kuisaidia kupambana na uasi.


Waziri mkuu wa Ethiopia Meles ZenawiPicha: AP Photo

Ethiopia iliyopeleka wanajeshi wake Somalia waliohudumu kwa kipindi cha miaka miwili imesema kuwa itaitikia mwito huo iwapo itatimiza wajibu huo katika misingi ya sheria za kimataifa. Hata hivyo, kulingana na wakazi wa maeneo ya mpakani, Ethiopia tayari imeshapeleka vikosi vyake Somalia.Kenya, kwa upande wake, ilitangaza Ijumaa iliyopita kuwa kamwe haitoruhusu hali ya nchi jirani yake kuvurugika, jambo ambalo huenda likasababisha machafuko katika eneo zima la Pembe ya Afrika. Moses Wetangula Waziri wa mambo ya nje wa Kenya alisisitizia''Ni wajibu wetu kama serikali na nchi kuyalinda maslahi yetu ukiwemo usalama nchini mwetu. Serikali na raia wa Kenya watahakikisha hilo linatimizwa ili kuhakikisha kuwa matukio ya Somalia hayatoiathiri amani na usalama wa Kenya kwa njia yoyote ile.''


Mwanzoni mwa mwezi wa Mei wanamgambo wa kiislamu walio na misimamo mikali walianzisha tangu mwanzoni mwa mwezi wa Mei harakati za kutaka kumng'oa madarakani Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed. Ifahamike kuwa uongozi wa muda wa Somalia unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa uliosimamia uteuzi wake. Katika kipindi cha siku chache zilizopita wanamgambo hao wameongeza mashambulizi dhidi ya uongozi huo, jambo lililosababisha vifo kadhaa. Mjumbe maalum wa Somalia katika Umoja wa Afrika, Nicholas Bwakira, anaeleza kuwa kundi hilo halina ajenda yoyote ya kisiasa''Kundi la Shabaab halina ajenda yoyote ya kisiasa.Lengo lao hasa ni kuua tu, hawana jengine la maana. Kundi hilo limekuwa likisajili wapiganaji kutoka Afrika, Asia, kwa hiyo tunatoa ishara maalum kuwa changamoto hii ni tishio la amani katika jamii ya kimataifa.


Vikosi vya Uganda vya AMISOM mjini MogadishuPicha: AP

Mpaka sasa takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa kiasi cha watu 300 wameuawa katika mashambulio hayo na wengine wapatao125,000 wameachwa bila makazi kwa kuyakimbia machafuko hayo. Baadhi ya waliouawa ni viongozi watatu wa ngazi za juu, akiwemo mbunge mmoja, waziri wa ulinzi, pamoja na kamanda wa ngazi za juu wa polisi.Waziri huyo aliuawa katika shambulio la bomu la kujitolea muhanga lililotokea kwenye hoteli aliyokuwako mjini Beledweyne.Itakumbukwa kuwa kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM, kilicho na wanajeshi 4,300 kinaendelea kushika doria mjini Mogadishu. Hii leo Umoja wa Afrika umerejelea kusisitiza kauli yake kuwa unaingiwa na wasiwasi na hali ya Somalia na umeunga mkono ombi la serikali yake la kutaka kusaidiwa. Katika taarifa yake Kamishna wa Umoja wa Afrika, Jean Ping, alisema kuwa serikali ya Somalia ina haki ya kuomba msaada kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja huo pamoja na jamii ya kimataifa.

Mataifa ya eneo hilo pamoja na yale ya magharibi yanahofia kwamba endapo ghasia zitaendelea Somalia, makundi yaliyo na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda huenda yakapata nguvu mpya na kulivuruga eneo lote hilo. Marekani imeliweka kundi la al Shabaab kwenye orodha yake mashirika ya kigaidi.

Wakati huohuo, katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, Conference, Ekmeleddin Ihsanoglu, ameitolea wito jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuingilia katika uasi huo.

Bwana Isanoglu amewatolea wito viongozi wa mataifa wanachama wa OIC kuipiga jeki serikali ya muda ya Somalia. Katika taarifa yake kiongozi huyo ameyashtumu mashambulio hayo ambayo ni kinyume na maadili ya dini ya kiislamu yanayosisitiza kudumisha amani na maridhiano.

Somalia ni mwanachama wa shirika hilo linalozileta pamoja nchi 57 wanachama.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE/ RTRE

Mhariri: Miraji Othman






Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW