Majeshi ya Korea kusini na Marekani yawekwa katika tahadhari ya juu.
28 Mei 2009Wizara ya Ulinzi ya Korea kusini imesema Vikosi vya Majeshi ya Anga na Ardhini vimewekwa katika hali ya tahadhari kubwa hususan katika maeneo ya mpakani ya ardhini na majini, baada ya taifa hilo la kikomunisti la kaskazini kutangaza kuachana na makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya Korea mwaka 1953.
Msemaji wa Jeshi la Korea Kusini Won Tae-Jae amesema jeshi bila ya huruma litashughulikia vikali hatua hiyo ya uchokozi ya Kijeshi ya Korea kaskazini.
Hasira za sasa za Korea kaskazini zimechochewa na uamuzi wa Korea kusini kujiunga na juhudi za kiulinzi zinazoongozwa na Marekani katika kuzuia ueneaji wa silaha za maangamizi, hatua ambayo inaweza kuzisimamisha na kuzikagua meli, licha ya Korea kusini kusema kwamba meli za biashara za kaskazini zinaweza kukatisha mipaka yake ya bahari chini ya mkataba wa mwaka 2005.
Hata hivyo Pyongyang imeuelezea uamuzi huo wa Seoul kwamba ni sawa na kutangaza vita.
Hali ya wasiwasi umeongezeka tangu Korea kaskazini ilipofanya jaribio lake la nyuklia siku ya Jumatatu, ambalo lilikuwa na nguvu zaidi ya lile lililofanyia mwaka 2006, na kufuatiwa na majaribio mengine matano ya makombora yake ya masafa mafupi.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, hii ni mara ya tano katika kipindi cha miaka 15 kwa Korea kaskazini kutishia kuvunja mkataba huo wa amani wa kusimamisha mapigano.
Marekani jana ilisisistiza nia yake ya kuzilinda Japan na Korea kusini dhidi ya kile ilichokiita vitisho vya Kijeshi vya Korea kaskazini.
Wanadiplomasia wa nchi za magharibi katika Umoja wa Mataifa wanasema kuwa mataifa yenye nguvu yameahidi kuweka vikwazo dhabiti dhidi ya Pyongyang.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton amesisitiza msimamo wa nchi yake kuwajibika kuzilinda Korea kusini na Japan.
Aidha amesema Pyongyang imeendelea kudharau Jumuia ya Kimataifa na kuendelea na maamuzi yake.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amesema muungano wa Jumuia ya Kimataifa, ikiwemo China na Urusi wanafanyia kazi hatua itakayochukuliwa na Umoja wa Mataifa kuiadhibu Korea kaskazini kufuatia jaribio lake la nyuklia siku ya Jumatatu.
Mwandishi: Halima Nyanza(AFP)
Mhariri: Abdul-Rahman