Majeshi ya Syria yaendelea kuuwa raia
25 Aprili 2011Aidha wanajeshi pia wamekishambulia kitongoji cha Douma, kilichoko katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus.
Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa zaidi ya watu 350 wameuawa na vikosi hivyo vya serikali tangu kuanza kwa machafuko nchini humo mwezi uliopita.
Idadi hiyo ya watu, wameuawa hii leo na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati majeshi ya Syria yalipofanya mashambulio katika mji huo wa Daraa ulioko kusini mwa nchi, kwa kutumia vifaru na askari doria.
Wakaazi wa mji wa Daraa, ambako harakati za upinzani dhidi ya Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad zilipoanza kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, wamesema wanajeshi takriban elfu 3, waliwasili katika mji huo mapema leo na kufanya mashambulio.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, nyumba za wakaazi zimekuwa zikifanywa hospitali, kwa ajili ya kuwatibu majeruhi.
Waandishi wengi wa habari wa kigeni wamefukuzwa nchini humo na kufanya kuwa ngumu kuthibitisha hali halisi katika eneo hilo.
Wakati huo huo, majeshi ya ulinzi ya Syria na watu walio na silaha wafuasi wa rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad, wameripotiwa pia kushambulia eneo kubwa la kitongoji hicho cha Douma na kuwapiga kwa risasi raia wa kawaida wasiokuwa na silaha pamoja na kuwakamata wakaazi wengine wa eneo hilo.
Wanaharakati wqa haki za binadamu wamesema watu kadhaa wamekamatwa na wengine kujeruhiwa na kuelezea kwamba wanajeshi wamekuwa wakifanya hivyo katika maeneo yote ambayo kuna machafuko ya kudai demokrasia na kwamba wanafanya hivyo ili kuyazima mapinduzi kwa kutumia mtutu wa bunduki.
Mawasiliano katika mji hio wa Douma yamekatwa, lakini wanaharakati walifanikiwa kukimbia katika kitongoji hicho baada ya mashambulio kuanza na kuripoti hali ilivyo.
Aidha wanaharakati wa haki za binadamu wamefahamisha pia vikosi vya jeshi la serikali na watu waliokuwa na silaha, wafuasi wa rais assad wamewapiga risasi na kuwaua raia 13 hapo jana katika mji wa Jabla ulioko katika pwani ya Mediterranean, ambako wanajeshi walipelekwa kufuatia upinzani uliotokea siku moja kabla.
Wanaharakati za haki za binadamu wamesema wanahofia kwamba majeshi yanayoongozwa na Rais assad yanajiandaa kufanya shambulio lingine katika mji wa Nawa, baada ya kuripotiwa mabuldoza na magari mengine ya kijeshi yakielekea huko.
Akizungumzia hatua ya jeshi kujiingiza katika operesheni za kuwazima waandamanaji hao wanaotaka mageuzi, Fares Braizat kutoka katika kituo cha utafiti na masuala ya sera kilichoko Doha Qatar ni kushindwa kwa utawala kuchukua hatua mbadala.
Katika mazishi ya jana ya waandamanaji waliouawa na wanajeshi, maelfu ya watu katika mji huo wametoa wito wa kutaka Rais Assad aondolewe madarakani.
Katika hatua nyingine, umeme na mawasiliano mengine yalikatwa jana katika baadhi ya maeneo ya mji huo wa Nawa, huku baadhi ya wanajeshi wakiweka vizuizi katika mitaa ya mji huo, ikiwa wanajiandaa kujilinda dhidi ya shambulio.
Mwandishi: Halima Nyanza:Reuters
Mhariri:Josephat Charo