Majeshi ya Syria yalipua ngome za waasi
12 Septemba 2016Shirika la uangalizi wa haki za binadamu limeripoti juu ya mashambulio ya mabomu yaliyofanywa na majeshi ya serikali kwa kutumia ndege za kivita katika maeneo ya wapinzani katika mji wa Endan uliopo kaskazini mwa Aleppo. Mji wa Aleppo ndio unaokabiliwa zaidi na machafuko nchini Syria.
Pia mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na wapinzani yamefanyika usiku kucha katika maeneo ya kusini-kaskazini mwa mji wa Aleppo na pande zote zimepata maafa kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo la uangalizi wa haki za binadamu lenye makao yake nchini Uingereza na ambalo hutegemea ripoti zake kutoka kwenye mtandao wake uliopo ndani ya Syria.
Mapigano hayo yamewasababishia watu taharuki kubwa ambapo wameshindwa kutoka majumbani mwao ili kwenda kusherehekea sikukuu ya Eid ul Adha inayoadhimishwa duniani kote leo hii. Rais Bashar Assad amehudhuria kwa nadra sala ya Idd katika msikiti uliopo nje kidogo ya mj wa Daraya. Mji huu ulijisalimisha mwezi uliopita baada ya kuzingirwa na majeshi ya serikali kwa miaka minne. Televisheni ya taifa ya Syria ilimwonyesha rais Assad katika msikiti wa Saad Bin Moaz. Kiongozi huyo aliungana pamoja na baadhi ya wanachama wa chama chake cha Baath pamoja na mawaziri na wabunge.
Kerry na Lavrov wafikia makubaliano ya kusitisha mapigano
Wakati huo huo makubaliano ya kusitisha vita nchini Syria baina ya Marekani na Urusi yanatarajiwa kuanza leo magharibi ijapo kuwa kuna taarifa tofauti kutoka kwa vikundi vya wa waasi ambapo baadhi yao wana tashwishi na makubaliano hayo. makubaliano hayo yamefanyika baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Maarekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov huko mjini Geneva. Makubaliano hayo yanaairuhusu serikali ya Syria kuendelea kuyashambulia makundi ya wapiganaji wa kundi linalojiita dola la Kiislamu IS na yale yanayounga mkono kundi la AlQaida hadi pale Marekani na Urusi zitakapochukua jukumu hilo baadae.
Uturuki nayo inajiandaa kupeleka zaidi ya malori 30 ya vyakula, nguo za watoto na vitu vya watoto vya kuchezea katika mji wa Aleppo. Rais Tayyip Erdogan amesmema makubaliano ya kusitisha mapigano ya saa 48 huenda yakaongezwa muda hadi wiki moja na labda muda zaidi kuelekea amani ya kudumu.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/AFP/AP/REUTERS
Mhariri:Yusuf Saumu