1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Ufaransa yapambana na waasi Mali

14 Januari 2013

Wakati majeshi ya Ufaransa yakipigana na waasi nchini Mali, waziri wa Ulinzi wa Ufaransa amesema waasi hao wameuteka mji wa Diabaly. Baraza la usalama la Niger linajadili juu ya hali ya usalama katika nchi jirani Mali.

Ndege ya kijeshi ya Mali
Ndege ya kijeshi ya MaliPicha: Reuters

Wapiganaji wenye itikadi kali ya kiislamu leo wameuteka mji wa Diabaly ulioko takriban kilometa 400 kaskazini mwa mji mkuu wa Mali, Bamako. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Ufaransa na maafisa wa usalama wa nchini Mali. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian ameeleza kwamba waasi waliuteka mji huo baada ya mapambano makali dhidi  ya wanajeshi wa serikali ya Mali. Chanzo kimoja cha habari kutoka Mali kimeeleza kwamba waasi waliingia katika mji wa Diabaly wakitokea kwenye eneo la mpaka kati ya Mauritania na Mali. Zaidi ya hayo, imeelezwa kwamba aliyeongoza mashambulizi ya mji wa Diabaly ni mtu anayefahamika kwa jina la Abou Zeid, ambaye ni kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda katika ukanda wa Maghreb. Hata hivyo, ndege ya kijeshi ya Ufaransa imefanikiwa kuwalenga waasi katika mji wa Douentza.

Majeshi hayo yaliingia Mali siku ya Ijumaa kupambana na waasi nchini humo na tayari baadhi ya wanajeshi hao wamepoteza maisha yao katika mapigano. Pia vipo vitisho vya kigaidi vinavyoifikia Ufaransa. Marc Trevidic kutoka taasisi ya kupambana na ugaidi nchini humo anaweka bayana kwamba anafahamu hatari inayoambatana na hatua ya nchi yake kupambana na waasi Mali: "Ni wazi kabisa kwamba kwa waasi wenye itikadi kali ya Kiislamu, maadui si Umoja wa Mataifa wala Waafrika. Hapana, Wafaransa ndio wapinzani wao. Kwa hakika watajaribu kufanya mashambulizi ya kigaidi. Lengo letu ni kuwazuia"

Waasi wa Ansar Dine nchini MaliPicha: Romaric Ollo Hien/AFP/GettyImages

Niger kutuma wanajeshi 500

Licha ya tishio hilo la kigaidi, rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amepongezwa na wengi kwa hatua hiyo ya kupambana na waasi. Wahariri wengi wa magazeti wanamsifia, wanasiasa wa vyama vyote vya Ufaransa wanasema kwamba hii ilikuwa hatua ya muhimu.

Naye rais Mahamadou Issoufou wa Niger, ambayo ni nchi jirani ya Mali, leo ameitisha mkutano wa baraza la usalama la nchi yake na kujadili suala la usalama wa Mali. Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la mawaziri nchini Niger ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wamefanya kikao kujadili hatua watakazochukua katika mzozo wa Mali. Niger imeahidi kupeleka wanajeshi 500 kuungana na kikosi cha kulinda usalama cha jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS.

Vyombo vya usalama vinaendelea kupambana na waasiiPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, viongozi wa vuguvugu la kudai eneo huru la Azawad wamekubali kuungana na majeshi ya Ufaransa kupambana na waasi. Msemaji wa kundi hilo la watu kutoka kabila la Tuareg ameiambia AFP kwamba wako tayari kushiriki katika vita dhidi ya ugaidi. Nao Umoja wa Ulaya umetangaza kwamba hautatuma wanajeshi kupambana na waasi Mali. Hadi sasa, umoja huo umeweka mipango ya kutuma wakufunzi watakaotoa mafundisho kwa wanajeshi wa Mali.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri: Saumu Yusuf