Jeshi la Ujerumani limewaondoa watu 101 kutoka Sudan.
24 Aprili 2023Ujerumani imewahamisha watu 101 kutoka Sudan. Jeshi la Ujerumani limesema hapo jana Jumapili ndege aina ya Airbus A400M iliyowabeba wajerumani walioondolewa kutoka Sudan ilitua salama nchini Jordan. Wakati huo huo serikali za nchi kadhaa zimewaondoa wanadiplomasia na watumishi wao waliokuwa wamekwama nchini Sudan.
Soma:Marekani yakamilisha kuwaondoa watu wake Khartoum
Mapigano hayo yanaendelea kwa wiki mbili sasa bila ya kuonesha dalili za kusimamishwa licha ya pande mbili zinazopingana hapo awali kukubaliana kuacha mapigano,kwa muda, kwa ajili ya siku kuu ya Eid.
Wizara za ulinzi na mambo ya nje za Ujerumani zimesema zinashirikiana na washirika wake na kwamba lengo ni kuwanusuru wajerumani kutoka kwenye eneo la vita lakini pia jeshi la Ujerumani litawahudumia raia wa nchi za Umoja wa Ulaya na wa nchi nyingine pia.
Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayesimamia Mambo ya Nje na Sera ya Usalama, Josep Borrell amesema wajumbe wa Umoja wa Ulaya wa nchini Sudan pia waliondolewa ulihamishwa salama siku ya Jumapili. Borrell aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa na Wizara ya Ulinzi ya nchi kwa kufanikisha zoezi hilo kwa msaada kutoka Djibouti. Borrell aliongeza kusema kwamba balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Sudan anaendelea kuhudumu katika nchi hiyo. Balozi huyo wiki jana alishambuliwa katika makazi yake wakati wa mapigano.
Soma:Papa Francis ahimiza mazungumzo kumaliza mzozo wa Sudan
Ujerumani imejiunga na nchi nyingine, kama Marekani, Ufaransa, Uholanzi na Ubelgiji, ambazo tayari zilianza kuwahamisha wafanyakazi wao wa ubalozi na familia zao.
Wakati huo huo kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa kukomesha umwagaji damu nchini Sudan. Alitoa wito huo wakati wa misa ya Jumapili kwenye uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro na amezitaka pande hasimu zifanye mazungumzo.
Vyanzo:/AFP/DW