Majeshi ya Ujerumani yaondoka Kunduz
20 Oktoba 2013Hatua hiyo inawakilisha hatua muhimu kuelekea kuondolewa kwa majeshi ya NATO nchini humo.
Miaka kumi baada ya Ujerumani kuanza kuweka majeshi yake katika jimbo lenye matatizo la kunduz ,jeshi la Ujerumani Bundeswehr limetangaza kuwa limefikisha mwisho ujumbe wake jana siku ya Jumamosi(19.10.2013).
"Tumekamisha kwa mafanikio operesheni ya "kujiondoa", amesema luteni kanali Heiko Diehl baada ya kuwasili katika kituo cha jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan katika mji wa Mazar-i-Sharif.
Kukamilika kwa hatua ya Ujerumani kuviondoa vikosi vyake pia kumesifiwa na kamanda wa eneo hilo wa jeshi la kimataifa linaloongozwa na NATO linalotoa msaada wa usalama kaskazini mwa Afghanistan, meja jenerali Jörg Vollmer.
Wajivunia mafanikio
"Tunajivunia kile wanajeshi wetu walichofanikisha katika jimbo la Kunduz hadi katika dakika ya mwisho walipokuwa hapo," amesema Vollmer.
Jeshi la Ujerumani Bundeswehr lilikabidhi rasmi kambi yao kwa jeshi la usalama la Afghanistan katika sherehe iliyofanyika hapo Oktoba 6.
Hata hivyo , operesheni za usafirishaji zilichukua muda zaidi, ambapo majeshi yaliwasili hatimaye katika mji wa Mazar-i-Sharif asubuhi ya Jumamosi.
Mlolongo wa magari 119 , ikiwa ni pamoja na magari chapa Marder ya kivita , na wanajeshi 441 wamesafiri kilometa 300 kwa siku mbili.
Kuwekwa kwa jeshi la Ujerumani katika jimbo la Kunduz kunawakilisha mara ya kwanza kwa majeshi hayo kuhusika katika mapambano tangu vita vikuu vya pili vya dunia.
Sherehe hapo kabla mwezi huu zilihudhuriwa na waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle na waziri wa ulinzi Thomas de Maiziere, ambaye alisema katika hotuba kuwa Kunduz ilikuwa "sehemu muhimu sio tu kwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, lakini pia jina Kunduz linabaki kuwa alama ya mashambulizi ya anga yaliyoamrishwa katika eneo hilo ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 100 na kuwajeruhi wengine 11 Septemba mwaka 2009, wengi wao wakiwa ni raia.
Msaada bado waendelea
Kwa hatua hiyo , kituo cha Mazar-i-Sharif kinakuwa cha mwisho kwa Ujerumani nchini Afghanistan. Hata hivyo operesheni katika jimbo la Kunduz bado zinaendelea , kutokana na kuwapo wanajeshi 300 wa dharura ambao watawekwa katika eneo hilo ili kusaidia majeshi ya Afghanistan.
Operesheni ya Kunduz imedumu takriban kwa miaka kumi kamili, ambapo vikosi vya kwanza vya ujerumani viliwasili katika eneo hilo Oktoba 25, 2003. Uwekaji wa jeshi hilo katika eneo hilo la jimbo jirani la Baghlan umethibitisha kuwa miongoni mwa maeneo ya hatari sana kwa majeshi ya Ujerumani, ambapo wanajeshi wengi waliuwawa kuliko kokote kwingineko.
Zaidi ya wanajeshi 3,800 wanabakia nchini Afghanistan , ambapo zaidi ya wafanyakazi 5,350 wa jeshi hilo wakiwa katika eneo hilo wakati operesheni hizo zikiwa katika kwango chake cha juu. Zaidi ya wanajeshi 1,400 wa Ujerumani walikuwa Kunduz kwa wakati mmoja.
Baada ya marekani na Uingereza, Ujerumani ndio ilikuwa inachangia wanajeshi wengi zaidi katika jeshi hilo la kimataifa linalosaidia kuweka usalama nchini humo.
Majeshi ya kimataifa yanatarajiwa kufikisha mwisho operesheni za mapambano mwishoni mwa mwaka 2014, na kusafisha njia baadaye kwa ujumbe wa msaada wa mafunzo kulisaidia jeshi la Afghanistan.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rc/mkg(AFP,DPA) DW-English web
Mhariri:Caro Robi