1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Urusi yaondoka Georgia

Charo, Josephat22 Agosti 2008

Marekani na Ujerumani zinasema hazijaona ushahidi wowote kudhihirisha kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Georgia.

Wanajeshi wa Urusi wakiondoka mji wa Gori nchini GeorgiaPicha: AP

Msafara mkubwa wa magari ya jeshi la Urusi umeonekana ukiondoka kutoka kambi ya kijeshi iliyo magharibi mwa Georgia kuelekea mpaka wa jimbo lililojitenga la Abkhazia leo mchana. Katika eneo la mashariki mwa Georgia majeshi ya Urusi yameondoka kutoka kwenye kituo cha upekuzi na eneo walilokuwa wakilidhibiti katika kijiji cha Igoeti, kilomita 50 tu kutoka mji mkuu wa Georgia, Tbilisi.

Kamanda wa jeshi la Marekani barani Ulaya jenerali John Craddock, amelaani kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Georgia akisema kunafanyika kwa mwendo wa kinyonga.

Mapigano makali kati ya Urusi na Georgia yalisababisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimu wengine maelefu kuachwa bila makaazi na kuwa wakimbizi.

Vita vilizuka baina ya nchi hizo mbili baada ya serikali ya Georgia mjini Tbilisi kujaribu kulichukua jimbo lake lililojitenga la Ossetia Kusini kati ya Agosti saba na nane na hivo kusababisha Urusi kuanzisha harakati kubwa ya kijeshi dhidi ya Georgia.

Urusi imesisitiza kuondoka kwa wanajeshi wake kutoka Georgia kunafanyika kama ilivyopangwa, lakini serikali ya Ujerumani mapema leo imesema haijabainika wazi ikiwa kuna wanajeshi wowote wa Urusi wanaondoka Geogia. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Thomas Steg, amesema haiwezekani kuwepo na eneo la usalama la kudumu katika ardhi ya Georgia litakalolindwa na majeshi ya Urusi.

Georgia inahofia kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Urusi katika ardhi yake ni njama ya Urusi kutaka kulipanua jimbo la Ossetia Kusini kwa kuyateka maeneo mengine zaidi yaliyo himaya ya Georgia.

Kumezuka utata kufuatia Urusi kutangaza inawaondoa wanajeshi kutoka Georgia. Mjumbe wa Georgia katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Kakha Lomaia, amesema vikosi vya Urusi vimeondoka mji muhimu wa Gori na wanajeshi wanaendelea kuondoka kutoka maeneo kadhaa waliyokuwa wakiyadhibiti.

Lakini nje ya mji wa bandari wa Poti katika bahari nyeusi, yapata kilomita 200 magharibi mwa eneo lililokumbwa na mapiganao, wanajeshi wa Urusi wameonekana wakitumia tingatinga kuchimba mtaro kwenye kituo cha upekuzi kinacholindwa na wanajeshi wa Urusi wakiwa na magari yasiyoweza kutobolewa na risasi.

Maafisa wa Marekani wanakuchukulia kuondoka kwa wanajeshi wa Urusi kutoka mji wa bandari wa Poti kuwa mtihani mkubwa kwa serikali ya mjini Moscow katika kutekeleza mkataba wa amani uliosimamiwa na Ufaransa.

Majeshi ya Urusi yanaondoka Georgia huku baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiwa limegawanyika kuhusina na azimio linalonuia kuumaliza mzozo baina ya Georgia na Urusi.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin amesema, ´´Kinachohitaji kufanyika ikiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linataka kuendelea kuwa na jukumu muhimu la kisiasa, ni kuliidhinisha azimio hili letu na halafu mambo mengine yakijitokeza, basi yatashughulikiwa.´´

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Alejandro Wolff kwa upande wake amesema azimio la Urusi halieleweki.

´´Maeneo ambako Urusi inataka kuendelea kubakisha wanajeshi wake na majumu watakayokuwa nayo wanajeshi hao hayajaelezwa waziwazi sambamba na vipengele sita vya azimio la Ufaransa linalotaka majeshi ya Urusi yaondoke Georgia kabla Agosti saba. Hatuwezi kukubalia maelezo yasiyoeleweka.´´

Urusi imeeleza nia yake ya kubakisha kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani katika eneo maalum la usalama linalopakana na jimbo la Ossetia Kusini na jimbo lengine linaloegemea upande wa Urusi la Abkhazia, kwa misingi ya mkataba uliofikiwa mnamo mwaka wa 1999.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW