Majeshi yapambana na waandamanaji Misri
5 Mei 2012Mapambano hayo makali ya mitaani yameongeza hali ya wasi wasi ya kuzuka kwa wimbi jingine la ghasia kuelekea katika uchaguzi ujao ambao ni wa kumchagua rais mpya ambaye atachukua nafasi ya rais aliyeondolewa madarakani mwaka mmoja uliopita Hosni Mubarak.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mpito nchini Misri ambacho kimeambatana na ghasia , Waislamu wenye imani kali , badala ya makundi ambayo hayafuati imani za kidini , wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya watawala wa kijeshi ambao wamekuwa wakishutumiwa kwa kujaribu kung'ang'ania madarakani.
Marufuku kulikaribia jengo la wizara ya ulinzi
Baraza la kijeshi limeweka amri ya kutotembea kuanzia mchana hadi alfajiri katika eneo linalozunguka wizara ya ulinzi, ambalo limekuwa sehemu ya mapambano kwa waandamanaji wenye hasira baada ya watu tisa kuuwawa siku ya jumatano, ambapo wengi wao walikuwa ni waungaji mkono wa mgombea ambaye ameenguliwa kutoka kundi la Waislamu wenye msimamo mkali.
Ghasia hizo zimeiweka kampeni ya uchaguzi wa hapo Mei 23 hadi 24 katika mtafaruku mkubwa, wakati wagombea wawili wanaoongoza pamoja na wagombea wengine kadha wakiahirisha kwa muda kampeni zao wakipinga hatua za jeshi kushughulikia hali hiyo.
Waandamanaji wakusanyika tena Tahrir
Maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika eneo la Tahrir mjini Cairo , sehemu ambayo imetumika katika vuguvugu la mapinduzi ya umma mwaka jana. Waandamanaji walikuwa ni pamoja na waungaji mkono wa kundi la udugu wa Kiislamu na Waislamu wa madhehebu ya Salafi, lakini pia vijana wanamapinduzi ambao waliongoza maandamano ya umma ambayo yalimuondoa madarakani rais Hosni Mubarak walishiriki.
Licha ya onyo kutoka kwa maafisa wa serikali dhidi ya kukusanyika, makundi hayo yaliandamana hadi katika wilaya ya Abbasiyah na kujiunga na hatua ya kukaa chini nje ya jengo la wizara ya ulinzi , ambalo hapo kabla lilikuwa limeshikiliwa na waungaji mkono wa mgombea uchaguzi wa kundi la Kiislamu Hazem Abu Islami.
Mwanasheria ambaye amegeuka kuwa mhubiri wa dini, Abu Ismail mfuasi wa imani kali ya kidini alienguliwa kutoka katika kinyang'anyiro cha urais kwasababu marehemu mama yake anadaiwa aliwahi kuwa na uraia wa nchi mbili Misri na Marekani , na kumfanya kutokubalika kisheria kushiriki katika kinyang'anyiro hicho cha urais chini ya sheria za uchaguzi. Amewahamasisha wafuasi wake kuingia mitaani . Tunakabiliwa na njama za kuharibu mapinduzi, amesema msemaji wake Gamal Saber alipozungumza na shirika la utangazaji la Al-Jazeera.
Mwandishi: Sekione Kitojo /ape
Mhariri : Stumai George