Maji salama ni haki ya binadamu
29 Julai 2010Azimio hilo liliungwa mkono na mataifa 122 na mengine 41 yaliisusia shughuli ya kulipigia kura.Hakuna taifa lolote lililolipinga azimio hilo.Kinyume na ilivyotarajiwa,baadhi ya mataifa tajiri yakiwemo Marekani,Uingereza,Australia,Canada,Japan,Korea Kusini na mengine ya Afrika kama Kenya,Botswana,Zambia,Ethiopia na visiwa vya Trinidad na Tobago yaliisusia shughuli hiyo.Balozi wa Bolivia katika Umoja wa Mataifa,Pablo Solon ambaye nchi yake iko mstari wa mbele katika harakati hizo alisisitiza kuwa,'Magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama na ukosefu wa huduma za usafi husababisha vifo vingi zaidi kote ulimwenguni.Ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa husababisha vifo vingi zaidi vya watoto ikilinganishwa na idadi inayofariki kwasababu ya athari za pamoja za magonjwa ya Ukimwi,Malaria na Ukambi,alieleza.
Hakuna uwiano
Akizungumzwa kwa niaba ya Marekani,John Sammis aliwaelezea wajumbe kuwa nchi yake ilitaraji kwamba ingekuwa sehemu ya azimio linaloziunga mkono harakati kuhusu masuala ya maji katika Baraza la Haki za Binadamu, zinazoendelea mjini Geneva,Uswisi.Kulingana na mjumbe huyo,azimio hilo kamwe haliielezei haki hiyo kama ilivyo halisi katika sheria za kimataifa.
Katika taarifa yake baada ya azimio hilo kupitishwa,Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la uangalizi wa masuala ya chakula na maji,Maude Barlow alitahadharisha kuwa tatizo ni kubwa na,'' Kutakuwa na uhaba mkubwa wa maji safi ikiwa hatutaacha kuyachafua mazingira.Tunakabiliwa na tatizo kubwa katika mazingira ukivizingatia vyanzo vya maji na lazima tuwache kuyachafua mazingira.Tunakabiliwa na uhaba wa maji salama kote ulimwenguni,alifafanua.
Hatua muhimu
Ijapokuwa azimio hilo bado halijakuwa makubaliano kamili ya kisheria,hatua hiyo ya kuliidhinisha ina umuhimu mkubwa katika harakati za kupambana na uhaba wa maji safi,salama na huduma za usafi.Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa,kiasi cha watu bilioni 2 ni wakazi wa maeneo yanayokumbwa na uhaba mkubwa wa maji na wengine bilioni tatu hawana uwezo wa kupata maji ya mfereji yasiyo kuwa kwenye maeneo ya umbali wa kilomita moja.Ifahamike kuwa serikali za Singapore,Ufilipino na Cambodia ,zinazoutambua umuhimu wa kusambaza huduma za usafi na maji kwa wakazi wake,zimekuwa zikiendelea na harakati hizo kabla hata ya jamii ya kimataifa kutangaza kuwa ni haki ya kibinadamu.Wajumbe hao waliwatolea viongozi wa serikali wa kuwajibika na kuwatimizia raia wao haki ya kupata maji safi na huduma za usafi kote ulimwenguni.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE-ZPR
Mhariri:Josephat Charo