Majirani wa Myanmar washinikiza Suu Kyi aachiwe huru
2 Machi 2021Akizungumza leo katika mkutano huo unaowashirikisha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 10 wanachama wa ASEAN, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Hishammuddin Hussein amesema uongozi wa kijeshi wa Myanmar unapaswa kutoa ushirikiano kuhakikisha makubaliano yanafikiwa na kwamba jumuia hiyo inaweza kusaidia kuondoa tofauti zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita. Hussein ameutaka utawala wa kijeshi kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Retno Marsudi ameitaka Myanmar kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kufungua milango yake kwa ajili ya jirani zake wa ASEAN ili kusuluhisha mvutano unaozidi kuongezeka na kupata suluhisho la amani.
''Mazingira mazuri kwa ajili ya mazungumzo lazima yatawale, ikiwemo kuwaachia wafungwa wa kisiasa. Mawasiliano ya moja kwa moja ya ndani na mazungumzo miongoni mwa wadau wa Myanmar siku zote ni chaguo bora. Hata hivyo, Indonesia ina uhakika kwamba ASEAN iko tayari kuwezesha mazungumzo kama haya, pindi itakapohitajika,'' alisisitiza Marsudi.
Marsudi amesema demokrasia inapaswa kurejeshwa Myanmar na Indonesia inasisitiza kwamba matakwa ya watu wa nchi hiyo lazima yaheshimiwe.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Vivian Balakrishnan amewataka washirika wa nje wa ASEAN kutoiwekea Myanmar vikwazo vya kiuchumi ambavyo vitawaumiza wananchi wa kawaida wa nchi hiyo. Balakrishnan amesema katika mazingira ya sasa wawekezaji wa nje, ikiwemo Singapore wanaanza kutathmini tena uwekezaji wao katika uchumi wa Myanmar.
Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video, pia umewashirikisha wawakilishi wa uongozi wa kijeshi, ikiwa ni siku mbili baada ya machafuko ya umwagaji damu yaliyosababisha vifo vya takriban watu 18, mauji yaliyolaaniwa vikali na jumuia ya kimataifa. Watu wengine 30 walijeruhiwa katika maandamano hayo ya ghasia Jumapili iliyopita kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Februari Mosi.
Soma zaidi: Watu 18 wauawa Myanmar
Kabla ya mkutano huo wa ASEAN, Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong alisema matumizi ya nguvu yanayofanywa na uongozi wa kijeshi nchini Myanmar dhidi ya waandamanaji hayakubaliki na Suu Kyi anapaswa kuachiwa huru.
Huku mkutano huo ukifanyika, polisi nchini Myanmar kwa mara nyingine tena wametumia mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji waliongia tena leo mitaani kupinga utawala wa kijeshi. Ghasia zimezuka na watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo kwenye mji wa kaskazini wa Kalay. Maandamano pia yamefanyika kwenye miji mikubwa ya Myanmar ya Yangon na Mandalay.
(DPA, AP, AFP, Reuters)