Majivu ya Fidel Castro kusafirishwa Santiago
30 Novemba 2016Baada ya mamia ya maelfu ya watu kuhudhuria misa ya wafu kwa mwanamapinduzi wa Cuba Fidel Castro, majivu ya marehemu huyo yanaanza kusafirishwa leo kutoka jiji kuu Havana hadi Santiago kufanyiwa mazishi hapo siku ya Jumapili. Huo ukiwa umbali wa kilomita 900. Maelfu kwa maelfu ya wacuba wanatarajiwa kuwa barabarani kushuhudia majivu hayo yatakapokuwa yakisafirishwa.
Mwili wa Fidel Castro aliyefariki akiwa na umri wa miaka 90, Ijumaa wiki jana, ulichomwa moto kulingana na matakwa yake. Majivu yake yatapitishwa katika miji kadhaa nchini humo kwa siku tatu kwanzia leo, kabla ya kufikishwa mji wa Santiago ambako ndiko atazikwa siku ya Jumapili.
Mji wa Santiago unaojulikana kama chimbuko la ukomunisti wa Cuba, ndiko mapinduzi yaliyoongozwa na marehemu Castro yalianzia mnamo mwaka 1953 na akachukua urais mwaka 1959. Hapo jana mamia ya maelfu ya waombolezaji walifika kumpa heshima za mwisho jijini Havana. Rais wa Bolivia ni miongoni mwa waliohudhuria misa hiyo na alisema: "Fidel hajafa kwa sababu wanaopigania uhuru hawafariki. Huyo ni Fidel. Hajafa kwa kuwa mawazo hayafi hasa mawazo yanayoleta ukombozi. Fidel hajafa kwa kuwa mapigano hayajaisha hasa mapigano dhidi ya utengano. Fidel ni kama yuko hai kuliko zamani akiendeleza vita kuokoa makazi yetu ya pamoja".
Mazishi yake yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa wakiwemo marais Nicolas Maduro wa Venezuela, Daniel Ortega wa Nicaragua, Evo Morales wa Bolivia na Rafael Correa wa Equador, kando na wakuu wa nchi za Amerika ya kusini na mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos.
Uhusiano wa Cuba na Marekani
Fidel Castro alitawala Cuba kwa miaka 47, hadi alipojiuzulu mwaka 2006 kufuatia hali yake ya kiafya, na kumkabidhi nduguye Raul Castro. Tangu wakati huo hajajitokeza hadharani japo inaaminika alikuwa na wasiwasi na uhusiano ulioimarishwa mwaka 2014 kati ya nchi yake na hasimu wao wa jadi Marekani. Haijabainika ikiwa uhusiano huo utaendelea kuimarika baada ya Januari rais mteule wa Marekani Donald Trump atakapochukua rasmi urais.
Akitoa hotuba ya rambirambi jijini Havana, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema "Cuba haikutafuta madini ya dhahabu, almasi au mafuta barani Afrika. Wacuba walitaka uhuru na mwisho wa unyanyasaji wa bara la Afrika kutumiwa kama kiwanja cha kuchezewa na nchi kubwakubwa huku watu wakiteseka".
Fidel Castro alipendwa na wengi duniani hasa Amerika ya kusini na Afrika, kwa kusimama dhidi ya Marekani, huku akizindua mipango ya elimu bure na huduma za afya bila malipo kando na kuwatuma madakitari wao katika mataifa mengine duniani kutoa misaada ya kiafya.
Lakini wengine walimshutumu kuwa kiongozi wa kiimla aliyevuruga uchumi kutokana na sera zake za usosholisti na kuwanyima wacuba haki za kibinadamu mfano uhuru wa kujieleza.
Mwandishi: John Juma/DPE/RTRE/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel