Makaazi ya waziri wa ulinzi yalipuliwa Afghanistan
4 Agosti 2021Naibu waziri huyo wa ulinzi aliyelengwa hakujeruhiwa katika shambulizi hilo ambalo wanamgambo wa Taliban wamedai kuhusika.
Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amesema kundi hilo liliyalenga makaazi ya waziri huyo usiku wa kuamkia leo akisema kulikuwa na mkutano muhimu uliokuwa unaendelea wakati huo.
Shambulizi hilo linaonyesha jinsi hali ya usalama nchini humo ilivyodorora na ni ishara kwamba Mji Mkuu Kabul uko kwenye hatari ya mapigano wakati wanamgambo hao wa Taliban wakiwa wanachukua udhibiti wa maeneo mengi. Eneo lilipofanyika shambulizi hilo halijakuwa na mapigano kama ilivyo katika sehemu zengine za nchi hiyo.
Shambulizi lilikuwa la kulipiza kisasi
Bismillah Khan Mohammadi ni Kaimu waziri wa ulinzi wa Afghanistan.
"Wananchi wenzangu, leo magaidi walio na kiu ya damu wamefanya shambulizi la kujitoa mhanga nje ya nyumba yangu. Kutokana na huruma ya Mungu, mimi pamoja na familia yangu hatukujeruhiwa wakati wa shambulizi hili ila bahati mbaya baadhi ya walinzi wangu wamejeruhiwa. Ningependa kuwahakikishia wananchi wenzangu, vitendo kama hivyo haviwezi kuiondoa azma na nia yangu ya kuwateteeni pamoja na nchi yangu," alisema Bismillah.
Msemaji wa Taliban Mujahid amesema shambulizi hilo lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa yale mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la kitaifa la Afghanistan katika mikoa kadhaa ambayo anasema yalisababisha vifo vya raia huku wengine wakiyakimbia makaazi yao.
Msemaji wa waziri wa ulinzi Afghanistan Mirwais Stanekzai lakini amesema kwamba wanamgambo wote 4 waliohusika katika shambulizi hilo waliuwawa kwa kupigwa risasi baada ya makabiliano ya masaa matano.
Taliban imezidisha kampeniy a mashambulizi tangu Aprili
Mapema Jumatano kumeshuhudiwa mlipuko mwengine karibu na jengo kuu la shirika la ulinzi la Afghanistan katika Mji Mkuu wa Kabul. Kulingana na polisi watu wawili pamoja na afisa mmoja wa usalama wamejeruhiwa katika mlipuko huo. Hakuna kundi lililodai kuhusika na mlipuko huo.
Tangu Aprili kundi la Taliban limezidisha kampeni yake ya mashambulizi ili kuiangusha serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na Marekani. Haya yanafanyika wakati majeshi ya nchi za kigeni yakiongozwa na Marekani yanaelekea kukamilisha kuondoka kwake nchini humo baada ya miaka ishirini ya vita.
Mapigano hasa yamekuwa makali katika mji wa Herat karibu na mpaka wa magharibi na Iran na pia katika miji ya Lashkar Gah na Kandahar katika eneo la kusini.