Makabila ya Darfur yanaweza kubadili mwelekeo wa vita Sudan
6 Julai 2023Vita kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi, RSF, vimesababisha maafa katika eneo la Darfur, ambapo wataalam wanahofia kuongezeka kwa mgawanyiko wa kikabila kunaweza kusababisha ghasia zaidi.
Katika video iliyotolewa Jumatatu, viongozi kutoka makabila saba makuu ya jimbo la Darfur Kusini waliwataka wanachama wao kulihama jeshi na badala yake wapigane upande hasimu wa RSF.
"Tangazo hili litakuwa na athari kubwa" katika vita vya Sudan, ambavyo vimeua karibu watu 3,000, alisema mwanahabari mkongwe wa eneo hilo Abdelmoneim Madibo.
"Kama ilivyo kwa El Geneina, litaigawa Darfur Kusini kati ya Waarabu na wasio Waarabu," aliiambia AFP, akimaanisha mji mkuu wa Darfur Magharibi ambao umekuwa eneo la umwagaji damu mkubwa na mashambulizi yanayolengwa kikabila.
Kikosi cha wanamgambo wa RSF kina chimbuko lake katika kundi la Janjaweed -- wanamgambo wa Kiarabu wanaoogopwa ambao walifanya ukatili mkubwa dhidi ya makabila madogo madogo yasiyo ya Waarabu huko Darfur kuanzia mwaka 2003.
Soma pia: Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF bado kizungumkuti
Wengi wanahofia kurudiwa kwa historia katika vita vya hivi vya karibuni, huku wakaazi na Umoja wa Mataifa wakiripoti kuwa raia wanalengwa na kuuawa kwa sababu ya ukabila wao na RSF na wanamgambo washirika.
Pande zote zawavutia vijana
Pande zote mbili zimewavutia kwa muda mrefu na vijana wa Darfur, ambako ni nyumbani kwa robo ya wakazi wa Sudan.
Lakini wataalam wanabainisha kwamba wakati vita tayari vimechukua mwelekeo wa kikabila katika eneo hilo, bado havijaathiri muundo wa vikosi, ambavyo vinajumuisha makundi ya Waarabu na wasio Waarabu.
Manaibu kamanda majeshi mjini Nyala na mkoa jirani wa Darfur Mashariki ni majenerali kutoka kabila la Waarabu la Misseriya. Wakati huo huo, vikosi vya jeshi vinahesabu maafisa kadhaa kutoka kabila la Rizeigat, analotokea Daglo miongoni mwa nyadhifa zao.
Viongozi wa makabila yote mawili walionekana kwenye video ya Jumatatu, wakihamasisha uungwaji mkono kwa RSF.
Bado hakujashuhudiwa utoro mkubwa kutoka jeshi. Hata hivyo, wachambuzi wanahofia msukumo wa kikabila unaweza kuleta matabaka zaidi ya kikabila.
Mtaalamu wa Darfur Adam Mahdi alisema tangazo hilo lina uzito mkubwa, akisema viongozi wa kikabila wanawakilisha "serikali halisi" katika eneo hilo na bila wao, "jeshi halina heshima au uhalali".
Soma pia:Miji ya Darfur yashambuliwa huku vita vya Sudan vikisambaa
Lengo la video ya Jumatatu, aliiambia AFP, lilikuwa kuchora mstari mchangani, kukata uandikishaji wa jeshi na "kueleza wazi utiifu" wa makabila haya kwa RSF.
Jeshi linaweza kujikuta likikabiliana na upande mpana ulioungana "na kulifursha nje ya Darfur Kusini, ambapo kambi zake nyingi zimeanguka," Mahdi aliiambia AFP. Majaribu yanaweza kuwa "kuyapatia silaha makabila mengine na kuanzisha vita vya uwakala," aliongeza.
Jeshi lapuuza miito ya viongozi wa kikabila
Chanzo cha kijeshi kilipuuzilia mbali wito huo wa kuasi na kuuataja kama "mkogo tu wa kutaka kuangazia na vyombo vya habari" na viongozi wa kikabila "kwa ajili ya maslahi yao", kikizungumza na AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu hakina mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Kwa sasa, alisema, maslahi hayo yanawiana na yale ya Daglo - ambaye "anajaribu kuthibitisha kuwa anaungwa mkono na makabila".
Lakini katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Darfur, ambako watu wa makabila ya Waarabu ndiyo wengi, wapiganaji wa ndani wamejiunga na vita kwa upande wa RSF, kulingana na wakazi kadhaa.
Adam Issa Bishara, mwanachama wa kabila la Rizeigat, aliiambia AFP kuwa anajiandaa kwenda kupigania RSF mjini Khartoum. "Hao ni binamu zetu, hatuwezi kuwatelekeza,” alisema.
RSF haijatangaza ni wanajeshi wake wangapi wameuawa katika mashambulio ya anga ya karibu kila siku kutoka vikosi vya jeshi mjini Khartoum.
Soma pia:Gavana wa Darfur awataka raia kubeba silaha na kupambana
Saa chache tu baada ya video ya Jumatatu kuonekana mtandaoni, mashahidi katika mji wa Darfur Magharibi waliripoti mashambulizi "ya watu wenye silaha kutoka makabila ya Kiarabu yanayoungwa mkono na RSF".
Wanaharakati kutoka Darfur Magharibi wameishutumu RSF kwa "kuwanyonga" raia kwa kuwa sehemu ya kabila la Massalit, mojawapo ya makabila makubwa yasiyo ya Kiarabu katika eneo hilo.
Watetezi wa haki, viongozi wa kikabila na makundi ya kimataifa wamelaani mauaji ya maafisa wa Massalit katika mji mkuu wa Darfur Magharibi wa El Geneina, ambao umeshuhudia mapigano mabaya zaidi katika vita vya sasa.
Waangalizi wa mambo wanasema kitovu cha mapigano huko Darfur - eneo lenye ukubwa sawa na Ufaransa - kinahamia Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini na mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan.
Chanzo: AFPE