Makabiliano mapya yazuka kwenye msikiti wa al-Aqsa
5 Mei 2022Polisi ya Israel imesema katika taarifa yake kwamba imeweza kutawanya dazeni kadhaa za iliowaita 'wafanyafujo', waliokuwa wakiwarushia mawe maafisa wa usalama. Mwandishi wa shirika la habari la AFP amesema ameshuhudia idadi kubwa ya askari polisi katika eneo la msikiti wa al-Aqsa, lakini shirika la hilali nyekundu la Wapalestina halijatoa taarifa yoyote juu ya waliojeruhiwa katika makabiliano ya leo.
Soma zaidi: Idadi ya waliojeruhiwa Jerusalem kufuatia vurugu yapita 300
Chanzo cha vurugu hizi mpya ni kufunguliwa tena kwa ziara za waamuni wa Kiyahudi katika eneo la msikiti huo ambao ndilo takatifu zaidi katika dini yao. Kwa siku kadhaa zilizopita Wayahudi walikuwa wamezuiliwa kuingia katika eneo hilo wakati wa sherehe za kuhitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu.
Nyakati muhimu za kidini kwa dini tatu kubwa
Ghasia hizi zimeshuhudiwa wakati Israel ikiadhimisha sikukuu ya kuundwa kwa taifa hilo, na ni marudio ya kilichojiri siku chache zilizopita wakati eneo hilo takatifu kwa dini tatu kubwa duniani, Uislamu, Ukristo na Uyahudi, likiwa kiini cha mvutano. Kwa wakati mmoja, Waislamu walikuwa katika mfungo wa Ramadhani, Wakristo wakisherehekea siku ya Pasaka, nao Wayahudi wakiadhimisha Pasaka ya upande wao ambayo ni tofauti na ile ya Wakristu.
Soma zaidi: Waumini Israel kurejea msikiti wa al-Aqsa
Wapalestina, wengi wao wakiwa Waislamu, wanakasirishwa na kuongezeka kwa idadi ya Wayahudi wanaolitembelea eneo msikiti wa al-Aqsa, ambalo kwa Wayahudi linajulikana kama Mlima wa Hekalu. Kulingana na makubaliano yaliyodumu kwa muda mrefu, Wayahudi wanaweza kulizuru eneo hilo lakini hawaruhusiwi kusali.
Taifa la Kiyahudi halitobadilisha hali ilivyo sasa
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid amesema taifa la Israel halina mpango wa kutaka mabadiliko katika makubaliano hayo.
Tangu katikati mwa mwezi Aprili, vurugu kati ya polisi wa Israel na Wapalestina ziliwajeruhi watu karibu 300, na kundi la Hamas linaloongoza katika Ukanda wa Gaza lilitishia kurusha maroketi kuilenga Israel na mahekalu ikiwa polisi wake wataendelea kuwashambulia Wapalestina kwenye eneo hilo linalobishaniwa.
Soma zaidi: Al-Aqsa: Waislamu watilia shaka hatua za Israel
Hali hii ya uhasama baina ya pande hizo mbili ilivurugika kuanzia Machi 22, baada ya washambuliaji wa Kipalestina kuwauwa Waisraeli 12 akiwamo afisa wa polisi, ambapo Wapalestina 26 na raia watatu wa Israel wenye asili ya Kiarabu walipoteza maisha katika operesheni ya kiusalama ya Israel.
-afpe,ape