1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Mgogoro wa kiusalama wazidi kuongezeka nchini Haiti

19 Januari 2024

Wananchi wamejitokeza kuandamana kumshinikiza waziri mkuu Ariel Henry aondoke madarakani baada ya kushindwa kuidhibiti hali ya ukosefu wa usalama

Waandamanaji wakikimbia mabomu ya kutowa machozi
Maandamano mjini Porta-Au-Prince mwaka 2023Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Makabiliano ya siku kadhaa yaliyosababisha umwagaji damu,  kati ya magenge tofauti  yenye silaha yamepamba moto katika mji mkuu wa Haiti Port-Au-Prince.

Haiti imetumbukia tena katika mgogoro wa kisualama,makabiliano makali baina ya magenge yenye silaha yanayohasimiana yakichachamaa katika mji mkuu Port-Au Prince,kwengine wananchi wanaandamana kuitaka serikali iwajibike kushughulikia mgogoro huo uliotanuka.

Milio ya risasi imesikika majira ya alfajiri ya leo Ijumaa katika wilaya ya Solino Kusini mwa mji mkuu huo huku moshi ukionekana kufuka na kuhanikiza kwenye anga la mji huo kwa  mujibu wa mwandishi habari wa shirika la AFP.Miongoni mwa waliokuwa kwenye maandamano ni mkaazi wa Port-Au Prince Rene August

"Tunawataka watu wa mji mzima wajitokeze.Jamhuri nzima inapaswa kusimama kumshinikiza waziri mkuu Ariel Henry ashughulikie suala hili. Hatuwezi tena kuvumilia ukosefu wa usalama unaosababishwa na magenge. Hakuna kinachofanya kazi,ikiwemo taasisi za kusimamia demokrasia. Tunataka kuona uchaguzi bila ya kuwepo magenge. Kiongozi mkuu wa nchi hivi sasa hata yeye anafungamana na magenge. Nchi nzima imegeuzwa kuwa ya magenge.''

Matairi yaliyochomwa moto na waandamanajiPicha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Wanachama wa magenge yanayoendesha shughuli zao katika mji jirani wa Bel Air wamekuwa katika mapambano kwenye eneo hilo tangu Jumapili iliyopita na walioshuhudia wamethibitisha kwamba baadhi ya watu wameuwawa,ingawa hawakutowa idadi ya wahanga.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mtandao wa kutetea haki za binadamu Pierre Esperance, takriban watu 20 wameuwawa tangu Jumapili na miongoni mwa wahanga hao ni watu walioteketezwa wakiwa majumbani mwao.

Wengine waliuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati wakijaribu kukimbia kushambuliwa.

Tangu mwanzoni mwa wiki hii mamia ya watu wamekuwa wakiandamana katika miji ya Jeremie, Miragoane na Ouanaminthe wakishinikiza waziri mkuu Henry ajiuzulu.

Kiongozi huyo aliingia madarakani baada ya kuuwawa aliyemtangulia Jovenel Moise mnamo mwaka 2021.

Moshi umetanda baada ya matairi kuchomwa motoPicha: Richard Pierrin/AFP/Getty Images

Soma pia: Mahakama Kenya yaongeza amri ya kuzuia polisi kupelekwa Haiti Waandamanaji wanamkosoa waziri mkuu Henry kwa kushindwa kuchukuwa hatua wakati nchi ikiwa imetumbukia kwenye matatizo ya kiuchumi,kiusalama na kisiasa ambayo yamechochea makundi ya magenge yenye silaha kupata nguvu zaidi.

Mwaka jana Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba magenge nchini humo yanadhibiti kiasi asilimia 80 ya mji mkuu.

Baraza la Usalama la Umoja huo likapitisha mnamo mwezi Oktoba mwaka jana hatua ya kupelekwa kikosi cha ujumbe wa kimataifa  kitakachoongozwa na Kenya kuisadia polisi ya Haiti,japo inaweza ikachukuwa miezi kadhaa kabla ya kikosi hicho kuwasili katika taifa hilo la Carribean.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW