1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi mengine ya halaiki yagunduliwa Canada

1 Julai 2021

Kundi moja la kiasili Canada limesema limegundua miili 182 katika makaburi yaliyokuwa karibu na shule moja ya bweni iliyokuwa inasimamiwa na Kanisa Katoliki.

Kanada Saskatchewan | Marieval Indian Residential School Friedhof
Picha: AFP

Watoto kutoka nchi za kigeni waliokuwa wametenganishwa na familia zao walikuwa wakiishi katika shule hiyo.

Kugunduliwa kwa makaburi hayo karibu na eneo la Cranbook, British Columbia, kunafuatia ripoti ya ugunduzi kama huo wa makaburi katika shule zilizokuwa zinaendeshwa na kanisa ambapo katika shule moja zaidi ya makaburi 600 yaligunduliwa na mengine 215 katika shule ya pili. Eneo la Cranbook liko takriban kilomita 840 mashariki mwa mji wa Vancouver.

Miili hiyo ni ya watu wa jamii ya Ktunaxa

Jamii ya Wacanada wa kiasili ya Lower Kootenay Band katika taarifa imesema ilianza kutumia teknolojia mwaka jana kuanza kutafuta eneo karibu na shule ya zamani ya Kimisheni ya Mtakatifu Eugene ambayo ilikuwa chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 1912 hadi miaka ya 1970. Taarifa hiyo imesema wamegundua miili ambayo ilikuwa kwenye makaburi ambayo hayakuwa na alama na baadhi ya makaburi yalikuwa na kina cha futi tatu tu.

Wanajamii wakiweka mataa sehemu palipogunduliwa makaburiPicha: Geoff Robins/AFP

Inaaminika kwamba miili hiyo ni ya watu wa jamii ya Ktunaxa na jamii nyengine ya Wacanada wa kiasili. Karibu robo tatu ya shule 130 za bweni zilikuwa zinasimamiwa na Kanisa Katoliki Canada huku zengine zikiwa chini ya usimamizi wa kanisa la Presbyterian, Kianglikana na Kanisa la Umoja la Canada.

Tangu kugunduliwa kwa makaburi hayo makanisa kadhaa kote nchini Canada yamechomwa. Makanisa 4 Katoliki katika maeneo ya vijijini kusini mwa eneo la British Columbia yamechomwa moto na kanisa moja la Kianglikana liliteketezwa hivi karibuni.

Kulikuwa na dhulma za kingono na dhulma nyinginezo dhidi ya watoto

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani uharibifu huo.

"Katika moyo wa maridhiano leo, ningependa pia kuzungumzia uchomaji na uharibifu unaolenga makanisa Katoliki kote nchini. Hivi sivyo tunavyostahili kufanya. Uharibifu wa maeneo ya ibada ni jambo lisilokubalika na ni sharti likome. Ni lazima tushirikiane kurekebisha makosa ya zamani," alisema Trudeau.

Waziri Mkuu wa Canada Justin TrudeauPicha: Sean Kilpatrick/ZUMAPRESS/picture alliance

Serikali ya Canada imekiri kwamba dhulma za kingono na dhulma zenginezo ni mambo yaliyokuwa yakifanyika mno katika shule hizo huku wanafunzi wakichapwa kwa kuzungumza lugha zao za kiasili.

Kabla taarifa za ugunduzi huu mpya wa makaburi, Waziri Mkuu Trudeau alisema ameagiza bendera ya nchi hiyo ipeperushwe nusu mlingoti leo kwa ajili ya kutoa heshima ya watoto wa kiasili waliofariki katika shule hizo.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameelezea kusikitishwa na jambo hilo na kutoa wito kwa uongozi wa kanisa na kisiasa Canada kutoa maelezo ya matukio hayo ya kusikitisha. Papa lakini hakuomba msamaha kama vile alivyotakiwa na jamii za kiasili Canada na serikali ya nchi hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW