1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi manne ya halaiki yagundulika mjini Uvira

25 Februari 2026

Mwezi mmoja baada ya kuondoka kwa waasi wa AFC-M23 kutoka mji wa Uvira katika jimbo la Kivu Kusini nchini DRC, makaburi manne ya halaiki yamepatikana yakiwa na miili ya watu ipatayo 170 iliyozikwa humo.

Ndoma 2023 | Makaburi ya watu wengi yaliyogunduliwa katika kijiji cha Ndoma, karibu na Beni
Makaburi ya watu wengi yaliyogunduliwa katika kijiji cha Ndoma, karibu na Beni 2023Picha: AP/picture alliance

Mashuhuda mbalimbali wanasema takriban makaburi manne ya halaiki yamegunduliwa, yakiwemo mawili yaliyokuwa na miili zaidi ya mia moja karibu na kambi ya kijeshi iliyokaliwa na AFC-M23 mnamo Desemba na January katika kitongoji cha Kilomoni ndani ya mtaa wa Kavimvira. Ugunduzi wa makaburi hayo umeamsha hasira na wasiwasi miongoni mwa wakaazi wa Uvira. 

Kaburi jingine liligunduliwa likiwa na takriban miili ishirini katika kitongoji cha Kilibula katika mtaa wa Kalundu, na la nne likiwa na miili karibu hamsini, limegunduliwa katika kijiji cha Kabimba kwenye umbali wa kilomita nane kusini mwa mji wa Uvira.

Makaburi ya halaiki ya Kilibula na Kabimba yaligunduliwa na wakazi ambao walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama. Wakazi hawa wa Uvira mashariki mwa Kongo wanasimulia kwa huzuni.

"Walikuwa wakiwalenga vijana fulani ambao walidai kuwa wanashirikiana na serikali," alisema mkaazi mmoja na mwingine akihoji kwamba "nyie mnaokuja kutawala watu bado mnaweza kuwaua? Kwa maoni yangu, hawa ndio tuliokuwa nao hapa Uvira; tulikuwa pamoja na waasi. Na ni serikali iliporejea ndipo ilipogundua makaburi haya ya halaiki."

Mabaki ya miili ya watu iliyogunduliwa Kibumba kusini mwa GomaPicha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Mkaazi mwingine aliyezungumza na DW amesema hivi, "tulikuta miili ya hapa na pale, na miili hii yote, kwa makumi au ishirini, ilizikwa kwenye shimo moja. Hadi leo, familia nyingi bado zinawatafuta wapendwa wao bila kujua kuwa wamekufa”.

Mji wa Uvira wageuka ngome ya operesheni za kijeshi

Tangu zaidi ya mwaka mmoja, mji wa Uvira umegeuka kuwa ngome kubwa na kituo cha ujasiri cha operesheni za kijeshi, na makao makuu ya wapiganaji wa Wazalendo, ukihifadhi pia uwepo mkubwa wa vikosi vya jeshi la Kongo na wanajeshi kutoka Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Burundi.

Wanaharakati wa mashirika ya kiraia wanakumbusha kuwa mji wa Uvira ulipotekwa na waasi wa AFC-M23, wavulana wengi walishukiwa kuwa wanamgambo wa Wazalendo, wanaounga mkono jeshi la Kongo.

Watetezi wa haki za binadamu Uvira wanashutumu hali ya kutisha. Ghislain Kabamba, mkurugenzi wa Kituo cha Kuchunguza Sheria, Haki na Utawala kwa Uwiano wa Kijamii nchini Kongo, anataka uchunguzi huru ufanyike, "watu hawawezi kuuawa kama wanyama na kuzikwa hivyo. Tunalaani vitendo hivi vilivyofanywa na uasi wa AFC/M23. Tunazitaka mamlaka zetu katika ngazi zote kufanya uchunguzi kubaini waliouawa na waliowaua wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.”

Picha: picture-alliance/AP Photo

Kauli ya Gavana wa Kivu Kusini

Gavana wa jimbo la Kivu Kusini chini ya utawala wa Kinshasa, Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki, anathibitisha ugunduzi huu wa kutisha, huku akinyoshea kidole uwepo wa waasi wa AFC/M23 katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Uvira.

"Makaburi ya halaiki ambayo ndiyo kwanza tumeshagundua : la kwanza lipo katika eneo la Kavimvira lenye miili 132 na jingine liko Kilomoni karibu na mpaka na Burundi yenye miili 31."

Haya yakijiri, Ujumbe wa pamoja kutoka MONUSCO, na Tume ya Kimataifa ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), uliwasili Uvira kwakutathmini hali ya mambo, kabla ya kupelekwa kwa tume ya Umoja wa Mataifa ya kufuatilia usitishaji mapigano na serikali ya Kongo na AFC-M23.

Hadi ijumaa, ujumbe huo utahakikisha kwamba juhudi za ufuatiliaji na uthibitishaji ni za kuaminika, salama, na uwezekano kiutendaji. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW