Makaburi ya halaiki yagunduliwa El Fasher Sudan
6 Novemba 2025
Maabara ya utafiti wa kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale(HRL) imesema imepata ushahidi unaoendana na shughuli za utupaji wa miili ambapo imebainisha uwepo wa makaburi ya halaiki kwenye msikiti mmoja pamoja na kwenye hospital ya watoto.
Pia imebainisha kuonekana kwa mitaro yenye urefu wa mita moja, pamoja na kutoweka kwa makundi ya vitu vinavyoendana na miili karibu na hospitali, msikiti na maeneo mengine katika mji wa El Fasher ikionesha kuwa miili iliyohifadhiwa karibu na maeneo hayo ilihamishwa baadaye.
Katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa la AFP, Nathaniel Raymond wa Maabara ya Utafiti wa Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale (HRL) amesema picha za angani ndiyo njia pekee ya kufuatilia mgogoro unaoendelea katika mji wa El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini. Katika taarifa yake, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema Umoja wa Mataifa unasikitishwa na matukio hayo ya ukatili dhidi ya binadamu nchini Sudan.
ICC: Kinachoendelea Sudan kinaweza kuwa uhalifu wa kivita
Otone "Tunasikitishwa sana na ripoti zinazoongezeka za ukatili mkubwa dhidi raia wakati mapigano yakiendelea katika Jimbo la Darfur Kaskazini.
Shirika la OCHA linaripoti walio ndani wamerekodi mauaji, unyanyasaji wa kingono, udhalilishaji, unyang'anyi na mashambulizi, miongoni mwa dhuluma nyingine za kupangwa, ikiwa ni pamoja na dhidi ya watu wanaokimbia mapigano baada ya wanamgambo wa RSF kuteka mji mkuu wa jimbo, El Fasher, wiki iliyopita."
Awali ofisi ya mwendesha mashtaka katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ilisema yanayoendelea Sudan yanaweza kuwa matendo ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita. Mnamo Oktoba 28, Chuo Kikuu cha Yale kilichapisha picha kutoka hospitali ya uzazi ya El-Fasher inayoonyesha "rundo la vitu vyeupe" ambavyo havikuwepo hapo awali na vilivyopimwa kati ya "mita 1.1 hadi 1.9" (futi 3.6 hadi 6.2) huku miili ya binadamu ikiwa imelala chini huku miguu imejikunja.
HRL imekuwa ikitahadharisha Umoja wa Mataifa na Marekani kuhusu maendeleo katika eneo El Fasher , huku ripoti zake zikiwa marejeleo ya kufuatilia hali ya mambo katika eneo hilo.