1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi ya pamoja yenye miili 50 yagunduliwa DRC

19 Januari 2023

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamegundua makaburi mawili ya pamoja yakiwa na takriban miili 50 ya raia.

DR Kongo | Unruhen in Nord-Kivu
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Makaburi hayo yamegunduliwa mashariki mwa taifa hilo, baada ya visa kadhaa vya mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na makundi ya wanamgambo.

Walinda amani hao waligundua makaburi hayo walipokuwa wakishika doria katika mkoa unaokumbwa na machafuko wa Ituri, kufuatia mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na wanamgambo wa CODECO.

Farhan Haq, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, amesema jumla ya miili 42, ikiwemo 12 ya wanawake na sita ya watoto, ilipatikana kwenye kaburi moja katika kijiji cha Nyamamba.

Soma pia: Polisi ya DRC yatawanya maandamano dhidi ya vikosi vya EAC

Ameongeza kuwa kaburi jingine la pamoja pia liligunduliwa katika kijiji cha Mbogi likiwa na maiti saba ya wanaume.

Haq ametaka uchunguzi kufanywa kubaini ikiwa vifo vya waliozikwa kwenye makaburi hayo, vilihusiana na mashambulizi eneo hilo.

"Ujumbe wa MONUSCO unausaidia mfumo wa mahakama wa Congo, kuchunguza mashambulizi na vilevile miito inayotolewa kwamba washukiwa wachukuliwe hatua za sheria,” Haq amesema hayo akirejelea operesheni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani.

Mzozo wa kijamii baina ya jamii mbili jirani (Lendu na Hema) mkoani Ituri umesababisha vifo na kuwaacha wengi wakiishi kwa wasiwasi.Picha: Tom Peyre-Costa/NRC

Katika wiki za hivi karibuni, mkowa unaozongwa na machafuko wa Ituri unaopakana na Uganda, umekumbwa na machafuko.

Kisa cha kuuawa kwa mwalimu mmoja wa jamii ya Lendu kilichochea mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa wanamgambo wa CODECO, wanaodai kuiwakilisha jamii hiyo.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na mzozo kati ya jamii za Lendu na Hema. Kati ya mwaka 1999 na 2003, mzozo huo ulisababisha vifo vya maelfu ya watu, hali iliyosababisha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Ulaya kupelekwa ili kutuliza machafuko.

Machafuko yalirejea tena 2017 kufuatia kuibuka kwa wanamgambo wa CODECO, wanaodai kuitetea jamii ya Hema.

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu mkoa wa Ituri Dieudonne Lossa, amesema zaidi ya raia 80 wameuawa tangu Januari eneo hilo.

Haq ametahadharisha kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama mkoani humo na kuongeza kuwa raia 195 wameuawa, 68 wamejeruhiwa na 84 wametekwa nyara kwenye mashambulizi yanayohusishwa na CODECO na makundi mengine yenye silaha.

(Chanzo: AFPE)