1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukahaba, uchimbaji wachochea kusambaa kwa mpox Kongo

Angela Mdungu
3 Oktoba 2024

Makundi ya makahaba na wachimba majini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa yanayochochea kuendelea kusambaa kwa virusi vya Mpox ambavyo viliathiri kwa kiwango kikubwa taifa hilo

Biashara ya ngono.
Mwanamke anaefanya biashara ya ngonoPicha: Yui Mok/PA/picture alliance

Mji wa Kamituga ni maarufu kwa migodi ya dhahabu. Kwa mujibu wa mamlaka za afya,  eneo hilo ndilo lililoanza kupatwa na maambukizi ya virusi vya Mpox tangu janga hilo lilipoikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Septemba. 

Mji huo uliokuwa umetelekezwa na makampuni ya Ubelgiji katika miaka ya 1990, umekuwa ukiwavutia wachimbaji wakubwa na madogo wa madini.

Una wakaazi wasiopungua 300,000 na majengo yake yamejaa msururu wa ofisi za  kuuza na kununua dhahabu, vifaa vya uchimbaji madini na kumbi za starehe.

Ukweli kuwa virusi vya mpox vinasambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine baada ya kugusana, unaifanya Kamituga kuwa mazingira mahsusi ya kusambaa kwa mpox.

Soma pia:Africa CDC: Zaidi ya dola milioni 800 zimeahidiwa kwa Afrika kukabiliana na Mpox

Baadhi ya wachimbaji wa madini huibuka mjini baada ya siku ndefu  migodini ili kutumia fedha zao huku wakitafuta wanawake, makahaba na pombe.

Mmoja wa wachimba migodi Bitama Sebuhuni aliyewahi kulazwa hospitali baada ya kupata maambukizi ya mpox anasema maisha katika mji wa Kamituga yanawasukuma watu kufanya dhambi.

Anaeleza kuwa mara nyingi alifanya ngono isiyo salama na wanawake kadhaa wanaojiuza bila kutumia kinga.

Baadhi ya wagonjwa waliambukizwa mpox kupitia ngono

Daktari Dally Muamba Kambaji wa hospitali binafsi ya ALIMA anabainisha kuwa karibu asilimia 20 ya wagonjwa walipatwa na maambukizi hayo kwa njia ya ngono. Anasisitiza kwamba kutumia kinga kama vile mipira ya kike na ya kiume hakuzuii mtu kupata maambukizi hayo. 

Daktari mwingine wa hospitali hiyo James Wakilonga Zanguilwa anasema walipoanza kubaini maradhi hayo waligundua vidonda visivyo vya kawaida katika ngo    zi ya meneja wa ukumbi mmoja wa starehe.

Waelimisha rika wakionesha kinga dhidi ya ngonoPicha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Walipoona kuwa baadhi ya wanawake wanaojiuza kwenye ukumbi huo nao wana aina hiyo hiyo ya vidonda, walianza kupaza sauti za tahadhari. Sifa Kunguja ni mmoja wa wanawake wanaouza miili yao katika eneo hilo. 

Soma pia:Chanjo za ugonjwa wa Mpox zaanza kutolewa Afrika

''Watu wameanza kunikwepa wakisema kuwa nina virusi vya mpox. Baadhi ya watu wananisalimu kama wakiwa karibu tu, na wengine wananikimbia. Baadhi ya wanaofahamu kuwa nilikuwa na maambukizi ya mpox huwa wananisema.

Ameongeza pia "kwa hiyo sasa sina wateja wengine na siwezi kukidhi mahitaji yangu. Nimepoteza kila kitu. Maisha yangu yamebadilika na sasa ni mateso tu."

Wanawake wanaojiuza katika eneo hilo wanaendelea kutamba Kamituga. Wana chama chao na wanachama wake wanatoka katika maeneo mbalimbali ya Kongo na hata nchi jirani.

Nicole Mubukwa ni mmoja wa wanawake hao anasema tangu mlipuko wa mpox ulipoanza wateja wamepungua kwa kiwango kikubwa.

Usiri watawala kwa walioambukizwa 

Wanawake hao wanasema kuwa wengi wa walioambukizwa mpox hawasemi kuhusu maradhi hayo kwa kuhofia kupoteza wateja ambao ndiyo chanzo kikubwa cha mapato yao wanayoyahitaji ili waishi.

Janga la homa ya nyani mkoa wa Kivu Kusini

04:02

This browser does not support the video element.

Mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Alice anasema ugonjwa wa mpox ni kama UKIMWI, kwani kila mtu anauficha.

Soma pia:Shirika la Gavi kununua chanjo 500,000 za Mpox kwa ajili ya Afrika

Meya wa Kamituga,  Alexandre Bundya M’pila anasema hivi sasa bado elimu zaidi inahitaji kutolewa na kwamba wanahitaji namna ya kufikia hatua ya kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.   

Licha ya barabara mbovu zinazounganisha Kamituga na maeneo mengine ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, virusi vya mpox vimeendelea kusambaa katika eneo lote la Kivu Kusini. Na sasa mkoa huo ulioathiriwa vibaya na ugonjwa mpox ndiyo kituo kikuu cha ugonjwa huo.