1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamada wawili wa Iraq wauwawa

27 Agosti 2015

Majenerali wawili wa jeshi la Iraq wameuwawa baada ya mtu anaedaiwa kuwa mpiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kujiripuwa kwa mabomu akiwa ndani ya gari katika mji wa Ramadi wa jimbo la Anbar.

Irak Anbar Provinz Militär Flüchtlinge Mai 2015
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

((Majenerali wawili wa jeshi la Iraq wameuwawa baada ya mtu anaedaiwa kuwa mpiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kujiripuwa kwa mabomu akiwa ndani ya gari katika mji wa Ramadi wa jimbo la Anbar. Eneo ambalo vikosi vinavyounga mkono serikali vinapambana na wanamgambo))

Vikosi vya jeshi na vya polisi ambavyo vinaungwa mkono na wanamgambo wa Kishia, wapiganaji wa kikabila wa madhehebu ya sunni pamoja na muungano wa kijeshi unaofanya mashambulizi ya anga na ambao unaongozwa na Marekani, wote wanapigana ili kuukomboa mji wa Ramadi kutoka kwa wapiganaji wenye misimamo mikali ya madhehebu ya sunni. Hata hivyo maendeleo ya mashambulizi ya kuukomboa mji huo, uliopo umbali wa kilomita 100 magharibi mwa Baghdad yamekuwa yakizorota.

Msemaji Mkuu wa opresheni ya pamoja Brigadia Jenerali Yahya Rasool amesema, Naibu kamanda wa opresheni ya jimbo la Anbar Meja - Jenerali Abdel Rahman Abu Ragheef pamoja na Brigadi Safeen Abdel majeed ambae ni mkuu wa kikosi maalum, waliuliwa katika shambulizi hilo katika eneo la Jerayshi kaskazini mwa mji wa Ramadi pamoja na watu wengine watatu.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-AbadiPicha: Reuters/K. al-Mousily

Rasool ameiambia televisheni ya taifa kwamba jeshi liliingilia kati gari hilo liliokuwa limesheheni vifaa vya miripuko lakini hilo ndilo lilowapelekea mauti yao baada ya gari hilo kuripuka. Watu wengine 10 wamejeruhiwa kutokana na shambulizi hilo.

Serkali itaongeza mashambulizi kumzidi adui

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao na wafuasi wa kundi la IS, kundi hilo limesema kuwa shambulizi lililenga makao makuu ya jeshi la Iraq, ili kulipiza kisasi cha mauwaji ya mpiganaji mkuu wa kundi hilo wakati wa mapigano ya hivi karibuni.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi amesikitishwa na mauwaji ya makamanda hao na amesema wataongeza nguvu ya kumshinda adui yao - ambalo ni kundi la IS - ili kulipiza kisasi kwa kila tone la damu.

Mbali na hilo katika shambulizi lengine watu watatu wameuwawa pia kupitia mtu aliyejitoa muhanga kwa kujiripua ndani ya gari, lilokuwa linalenga kituo cha ukaguzi cha polisi ndani ya mji wa Bajwa, kilomita 15 kaskazini-magharibi mwa Kirkuk. Lakini hadi sasa hamna aliyejitokeza kuhusika na shambulizi hilo.

Kundi la IS liliuteka mji wa Ramadi mapema mwaka huu, na pia linadhibiti mji mwengine wa karibu wa Fallujah.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/eap/rtre

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW