1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiChad

Makambi ya wakimbizi Chad yakabiliwa na mzozo wa kiutu

22 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa makambi ya wakimbizi yaliojazana mashariki mwa Chad yanatazamiwa kuishiwa msaada na kuzidisha mzozo mbaya wa kibinadamu uliosababishwa na kuenea kwa vita nchini Sudan.

Kambi ya wakimbizi waliokimbia mapigano Sudan
Wakimbizi waliokimbia mapigano Sudan wakiwa wamekusanyika kambi ya Zabout huko ChadPicha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa unasema mzozo mbaya kati ya majenerali wanaohasimiana nchini Sudan umesababisha vifo vya zaidi ya watu 5,000 nchini humo, na kuwahamisha zaidi ya milioni tano. Nchini Chad, idadi ya wakimbizi imeongezeka na kuwa kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 20.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa vita nchini Sudan vinaelekea kuwa mzozo mbaya zaidi wa njaa duniani, ambapo theluthi moja ya watu milioni 18 nchini humo wakikabiliwa tayari na uhaba mbaya zaidi wa chakula.Kiongozi wa upinzani Chad auawa katika shambulizi makao ya chama

Kwenye kambi za wakimbizi mashariki mwa Chad, ukosefu wa maji salama ya kunywa na usafi vinasababisha kusambaa kwa magonjwa hatari. Shirika la misada la Madaktari Wasio na Mipaka, limesema limerikodi takribani visa 1,000 vya hepatitis E katika makambi na wanawake kadhaa wajawazito wamefariki.

Wakimbizi waliokimbia mapigano SudanPicha: MOHANED BELAL/AFP

Mratibu wa kikanda wa shirika hilo Erneau Mondesir, alisema hali ni mbaya sana katika makambi, na kuongeza kuwa bila hatua za haraka za kuboresha miundombinu ya usafi na kuboresha upatikanaji wa maji safi, kuna hatari ya kuongezeka kwa magonjwa yanayozuwilika na vifo.Chad yafanya kura ya maoni kuamua kuhusu rasimu ya katiba

Katika kambi ya Metche inayowahifadhi wakimbizi karibu 40,000, watu wana uhitaji mkubwa wa maji, chakula, hifadhi na usafi wa msingi. Uhaba wa maji unasababisha kusambaa kwa magonjwa, na wafanyakazi wa misaada wanahofia janga ikiwa ugavi utaisha. Marie Jose Alexander ni mratibu wa ushirikiano.

"Kutokana na upatikanaji mdogo wa maji bila shaka kuna magonjwa mengi yatokanayo na maji kama vile kuharisha, kipindupindu, na magonjwa mengine yanayohusiana na kuwa katika maeneo yenye msongamano wa watu na ukosefu wa huduma za vyoo," alisema Alexander.

Hali ya usalama: Chad iko katika hali ya tahadhari baada ya shambulizi kwenye idara ya usalama

Wakimbizi waliokimbia mapigano Sudan wakipanda gari kuelekea kambi ya mudaPicha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Wachambuzi pia wanahofia kwamba mzozo unaweza kuenea pia nchini Chad, ambako mvutano wa kisiasa ni mkubwa, kufuatia mauaji ya mwezi Februari, ya kiongozi wa upinzani, Yaya Dillo, katika mji mkuu. Alikuwa binamu wa rais na mshindani mkubwa katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Mei.Watu kadhaa wauawa Chad

Fedha na ugavi wa misaada katika shughuli za kibinadamu viko chini sana, hali ambayo mchambuzi mkuu wa taasisi ya utafiti ya Verisk Maplecroft, anasema itaongeza ushindani wa rasilimali kati ya wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi mashariki mwa Chad, na hivyo kuchochea zaidi mivutano ya ndani na kukosekana kwa utulivu wa kikanda

Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Deby Itno, alinyakua madaraka baada ya babake ambaye alieiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu kuuawa akipambana na waasi mwaka 2021. Mwaka jana, serikali ilitangaza kuongeza muda wa kipindi cha mpito cha miezi 18 kwa miaka miwili zaidi, hatua iliyosababisha maandamano nchi nzima.