1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamo wa rais wa Marekani ziarani Afghanistan

Hamidou, Oumilkher20 Machi 2008

Dick Cheney na Hamid Karzai wahimiza wanajeshi wa NATO wazidishwe Afghanistan

Makamo wa rais wa Marekani Dick Cheney akizungumza na rais Hamid Karzai mjini KabulPicha: AP



Makamo wa rais wa Marekani Dick Cheney na rais Hamid Karzai wa Afghanistan kwa pamoja wamewatolea  mwito wanachama wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wazidishe juhudi zao za kuhakikisha usalama na kuijenga upya Afghanistan inayokumbwa na machafuko ya umwagaji damu.



Makamo wa rais wa Marekani Dick Cheney amewasili kwa ghafla hii leo mjini Kaboul-katika juhudi za maandalizi ya mkutano wa kilele wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,mapema mwezi ujao mjini Bucharest ambako anataraji wanachama wa NATO watazidisha michango yao ya hali na mali nchini Afghanistan.


"Marekani na wanachama wengine wa ushirika wanabidi kua na wanajeshi wanaotosha kudhamini usalama" amesema makamo wa rais wa Marekani mbele ya waandishi habari,baada ya kuonana na rais Hamid Karzai wa Afghanistan.


"Tunahisi juhudi zetu lazma ziendelezwe na ziimarishwe"-ameongeza kusema makamo huyo wa rais wa Marekani.


Machafuko ya wataliban yanazidi kuenea nchini humo na mwaka jana visa vyao viligharimu maisha ya zaidi ya watu 8000,1500 kati yao ni raia wa kawaida.Umoja wa mataifa unakadiria mashambulio 160 ya kuyatolea mhanga maisha yamefanyika katika kipindi hicho hicho nchini humo.


Kutokana na hali hiyo inayozidi kua mbaya,jumuia ya kujihami ya magharibi NATO na hasa Canada wamekua wakiwashinikiza washirika wao wazidishe idadi ya wanajeshi wao hasa katika maeneo ya kusini.


Kwa upande wake rais Hamid Karzai amesisitiza vikosi vya usalama vya Afghanistan havina bado uwezo wa kutekeleza jukumu lao kikamilifu bila ya msaada wa wanajeshi kutoka nje.


"Siku itawadia ambapo Afghanistan itamudu kudhamini usalama wake na kulinda mipaka yake.Lakini sio sasa hivi-amesema kwa upande wake rais Karzai mbele ya waandishi habari.


Ziara ya makamo wa rais wa Marekani

haijalengwa maandalizi ya hujuma za akijeshi dhidi ya Iran-amesema mshauri mmoja wa makamo wa rais wa marekani ambae hakutaka jina lake litajwe.


Kwa upande mwengine lakini Dick Cheney ameelezea matumaini ya kuiona serikali mpya ya Pakistan ikiwa "rafiki na mshirika timamu wa Marekani,kama ilivyokua serikali iliyotangulia.


Ziara ya makamo wa rais wa Marekani haikutangazwa hapo awali kutokana na sababu za usalama.Katika ziara yake ya mwisho mjini Kaboul,mwezi february mwaka jana,mtu mmoja alijiripua karibu na kambi ya kijeshi ya Marekani alimokuwemo Dick Cheney na kusababisha watu 20 kupoteza maisha yao.


Makamo wa rais wa Marekani amepangiwa kuonana na wakuu wa vikosi vya nchi shirika vinavyoongozwa na Marekani na vile vya kimataifa vya ISAF vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya magharibi NATO.


Ziara ya Dich Cheney imefanyika katika wakati ambapo Irak inaadhimisha miaka mitano tangu ilipovamiwa na vikosi vya Marekani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW