1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rigathi Gachagua amshutumu bosi wake Ruto kwa ukatili

20 Oktoba 2024

Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amemshutumu Rais William Ruto kwa ukatili baada ya kuondolewa madarakani na Seneti. Gachagua alisema ulinzi wake umeondolewa na maisha yake yanaweza kuwa hatarini.

Kenya Nairobi | Mkutano wa Kilele wa Tabianchi Afrika 2023 | Rigathi Gachuaga akikaa kando na Rais William Ruto.
Rais William Ruto na Makamu wake Rigathi Gachagua wakiwa pamoja katika hafla ya zamani, huku uhusiano wao ukizidi kuharibika kutokana na mvutano wa kisiasa unaoendelea.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Makamu wa Rais wa Kenya aliyeng'olewa madarakani, Rigathi Gachagua,Jumapili alimshutumu vikali bosi wake, William Ruto, kuwa katili mkubwa, akionya kwamba maisha yake yanaweza kuwa hatarini.

Gachagua aliondolewa madarakani na Seneti kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake Alhamisi, lakini agizo la mahakama limesitisha mchakato wa kumteua mrithi wake.

"Nimeshtushwa na jinsi mtu niliyemsaidia kuwa rais, niliyekuwa na imani naye, na nilieteswa kwa kumsaidia, anavyoweza kuwa na ukatili mkubwa dhidi yangu," aliwaambia waandishi wa habari.

Gachagua mwenye umri wa miaka 59, aliyekumbwa na mzozo, alisema ulinzi wake umeondolewa na wafanyakazi wake wote wamepewa likizo ya lazima.

Bunge la Kenya lilipiga kura kumuondoa Gachagua na kisha kupeleka mashtaka 11 dhidi yake mbele ya Seneti, ambayo ilitibitisha mashtaka matano yaliopelekea kumuomndoa.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Amwajibisha Ruto kwa lolote litakalomtokea

"Ikitokea chochote kwangu au kwa familia yangu, Rais William Ruto lazima awajibishwe," alisema, akidai kuwa kumekuwa na majaribio ya awali ya kumuua.

Alikuwa akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali katika jiji kuu la Nairobi, ambako alikuwa akipatiwa matibabu kwa maumivu makali ya kifua.

Soma pia: Ruto amteua Kindiki kuwa naibu mpya wa rais wa Kenya

Gachagua aliugua Alhamisi, takriban saa moja kabla ya kutoa ushahidi katika kesi ya kihistoria ya siku mbili ya kumng'oa madarakani.

Baraza la juu la bunge liliendelea na upigaji kura wa kumwondoa ofisini baada ya mawakili wake kushindwa kuahirisha kikao hicho.

Alipatikana na hatia kwa mashtaka ikiwa ni pamoja na kutishia majaji na kueneza siasa za mgawanyiko wa kikabila, lakini alisafishwa kwenye mashtaka ya ufisadi na utakatishaji fedha.

Rigathi Gachagua na William Ruto wakiwa kwenye kampeni za uchaguzi wa 2022.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Uchaguzi wa Mrithi na Hatua za Mahakama

Katika sakata hiyo ya kisiasa inayobadilika kwa kasi, Ruto alimteua mara moja Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, kuchukua nafasi ya Gachagua.

Hata hivyo, Mahakama Kuu katika mji mkuu ilisitisha mchakato wa uteuzi huo dakika chache baada ya bunge kupiga kura kwa wingi kumuidhinisha Kindiki, msomi mwenye umri wa miaka 52 aliyebadilika na kuwa kiongozi mashuhuri wa kisiasa.
Jopo la majaji watatu linasubiri kusikiliza kesi hiyo Jumanne.

Soma pia: Kindiki: Msomi mnyenyekevu aliyegeuka kuwa kigogo wa kisiasa

"Rais, kwa kukiuka kabisa agizo la mahakama, ameondoa ulinzi wangu kwa ukatili," alisema Gachagua, licha ya yeye bado kuwa makamu wa rais.

"Sielewi ukatili wa aina hii... wakati mtu akiwa kwenye hali ya chini kabisa maishani na akijitahidi kwa kila hali kuendelea kuishi, unamfanyia ukatili mkubwa kama huo."

Mfahamu Kithure Kindiki mrithi wa Gachagua

02:17

This browser does not support the video element.

Ruto bado hajatoa tamko lolote hadharani kuhusu kumwondoa Gachagua madarakani.

Gachagua ni makamu wa rais wa kwanza kuondolewa madarakani kwa njia hii tangu kuanzishwa kwa sheria ya kumwondoa madarakani katika katiba mpya ya Kenya ya mwaka 2010.