1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamala Harris nchini Ghana kuanza ziara yake barani Afrika

27 Machi 2023

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris anayefanya ziara barani Afrika leo Jumatatu atakutana na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na siku ya Jumatano anatarajiwa kuzuru Tanzania na kisha atakwenda Zambia.

Ghana | US Vize Präsidentin Kamala Harris in Accra
Picha: Misper Apawu/AP Photo/picture alliance

Ziara yake hiyo inakusudiwa kuonyesha uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wa Afrika Magharibi ambaye anakabiliwa na kuongezeka shinikizo kutoka kwa wananchi wake ambao wanaonesha kutoridhika na hali ya mfumuko wa bei na wasiwasi mpya kuhusu usalama wa kikanda.

Kamala Harris ndiyo kwanza anaanza ziara yake hiyo ya wiki nzima katika bara la Afrika ambapo atazuru pia nchi za Tanzania na Zambia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuongeza mahusiano kati ya Marekani na nchi za Afrika wakati ambapo China na Urusi zinafurahia ushawishi mkubwa barani Afrika.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris mara alipowasili mjini Accra, Ghana.Picha: NIPAH DENNIS/AFP/Getty Images

Baada ya kupokelewa mjini Accra hapo jana Jumapili makamu huyo wa rais wa Marekani Kamala Harris alidokeza azma ya ziara yake akisisitiza kuwa Marekani inatarajia kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia katika bara hilo. Vilevile Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris atatangaza msaada wa kitita cha dola milioni 139 milioni kwa Ghana kwa mwaka ujao wa 2024.

Makamu wa Rais wa Marekani atafanya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na kisha atakutana na wawakilishi wa mashirika ya kiraia. Siku ya Jumatano Kamala Harris ataondoka mjini Accra kuelekea Dar es Salaam, Tanzania katika muendelezo wa ziara yake ya barani Afrika.

Soma:Makamu wa Rais wa Marekani awasili nchini Ghana

Safari ya Kamala Harris nchini Ghana, Tanzania na Zambia hadi Aprili 2 inafanyika baada ya mkutano wa kilele wa mwezi Desemba mwaka uliopita ulioandaliwa na Rais wa Marekani, Joe Biden mjini Washington ambapo viongozi wa Marekani na wenzao kutoka barani Afrika walikutana.

Ushawishi wa China barani Afrika unaleta wasiwasi mkubwa kwa sera ya mambo ya nje ya Marekani, na vilevile wasiwasi huo unaongezeka wakati ambapo Urusi nayo inaendeleza ushawishi wake barani Afrika kutokana na baadhi ya nchi za Afrika ambazo zina uhusiano wa muda mrefu na Urusi kuanzia enzi za Sovieti. Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Urusi, amefanya safari nyingi katika bara hilo katika juhudi za kuonesha kwamba nchi za Magharibi zimeshindwa kuitenga Urusi tangu nchi hiyo ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akiwa mjini Accra, Ghana.Picha: NIPAH DENNIS/AFP/Getty Images

Ziara ya makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris nchini Ghana pia inakusudia kuonesha jinsi Marekani inavyomuunga mkono Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo mmoja kati ya viongozi waliosimamia vyema uchumi wa nchi yake ulionawiri kwa kasi kabla ya janga la COVID-19 kukumba dunia. Hali hiyo imesababisha kupanda sana kwa gharama za chakula na mahitaji mengine ambayo yamekuwa yakiongezeka kila uchao jambo ambalo limeifanya Ghana kukabiliwa na mgogoro wa madeni wakati ambapo nchi hiyo inahangaika kulipa madeni hayo.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akiwa nchini Ghana pia anatarajiwa kukutana na wafanyabiashara, wanafunzi, wanawake na wakulima na pia atatembelea jumba la kihistoria la Cape Coast ambako watumwa waliwekwa miaka 400 iliyopita.

Vyanzo: AP/AFP/RTRE