Makamu wa Rais wa Marekani kuanza ziara yake barani Afrika
24 Machi 2023Ziara hiyo inajiri wakati ambapo Marekani ikitaka kujionesha kama mshirika bora kuliko China kwa bara hilo. Makamu huyo wa rais wa Marekani atafanya majadiliano kuhusu kujiingiza kwa China katika masuala ya teknolojia na uchumi barani humo, hatua ambayo inaipa wasiwasi nchi yake.
Marekani pia inakhofia kujiingiza kwa nchi hiyo ya Asia yenye nguvu katika suala la kufanya mabadiliko ya mfumo wa ulipaji madeni kwa nchi za Kiafrika.
Soma pia: Biden: Afrika inastahili dhima kubwa zaidi duniani
Moja wa nchi ambazo Kamala Harris atazitembelea ni Zambia ambayo ni ya kwanza katika bara hilo kutangazwa muflisi na kushindwa kulipa madeni yake ya nje wakati wa kipindi cha janga la korona, na iko kwenye mazungumzo na wakopeshaji wake ikiwemo China, kufikia makubaliano.
Kamala Harris atakwenda pia Ghana na Tanzania. Rais wa Marekani Joe Biden nae pia anatarajiwa kulizuru bara hilo mwishoni mwa mwaka huu.