Makanisa Kenya yaingilia kati mgogoro wa IEBC
18 Mei 2016Picha za ukatili wa maafisa wa usalama zilizosambaa katika mitandao ya kijamii baada ya maandamano ya tatu ya kupinga tume huru ya uchaguzi na mipala IEBC siku ya Jumatatu zimeibua hisia mbali mbali miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu na jumuia ya kimataifa kwa ujumla.
“Tume hii imesikitishwa hasa na vitendo vya polisi waliowakusanya waandamanaji na kuwapiga hadi kuwajeruhi,” alisema mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya haki za binaadamu nchini Kenya Kagwira Mbogori.
Marekani nayo kupitia Ubalozi wake mjini Nairobi imelaani vitendo vya ukatili wa polisi katika taarifa yale kwa vyombo vya habari na kutoa mwito kwa idara za usalama kuzingatia haki za binadamu kuambatana na katiba ya Kenya wakati wanapokabiliana na waandamanaji.
Polisi kuchunguza
Msemaji wa Polisi George Kinoti alisema jeshi hilo limeunda kamati ya uchunguzi kushughulikia malalamishi hayo. “Afisa yeyote ambaye atabainika alihusika katika ukiukaji wa sheria kinyume na kanuni zetu atakabilia vilivyo na hatua itachukuliwa dhidi yake,” alisema Kinoti.
Viongozi wa makanisa wamejitosa katika mgogoro huo kujaribu kuleta upatanishi kati ya upinzani na muungano tawala wa Jubilee juu mgogoro uliopo.
"Nakuwa na hofu kuona watu wanaanza kujeruhiwa, mali znaharibiwa na tunataka suluhu ipatikane kwa haraka, watu waache maandamano kwa sababu wanazungumza," alisema katibu mkuu wa Baraza la Makanisa nchini Kenya Askofu Peter Karanja.
Siku ya Jumatatu watu kadhaa walijeruhiwa huku wengine watatu wakihofiwa kufariki wakati polisi wa kukabiliana na ghasia waliposambaratisha maandamano ya upinzani dhidi ya tume ya uchaguzi. Hata hivyo mmoja wa waliodaiwa kufariki alijitokeza kwa vyombo vya habari akiwa hai.
Raila asisitiza kuendeleza maandamano
Upinzani umeapa kuendelea na maandamano hayo hadi pale mwenyekiti wa IEBC Isaac Hassan na makamishna wake watakapong'atuma mamlakani. "Maandamano yetu yataendelea kila Jumatatu hadi pale upande wa pili utakapokuwa tayari kwa mazungumzo," alisisitiza kiongozi mkuu wa muungano wa CORD Raila Odinga.
Upinzani unasema hauna imani na tume hiyo ya uchaguzi na kwamba uchaguzi mkuu mwaka ujao hautakuwa huru na haki chini ya usimamizi wa tume ya sasa.
Vyama vya KANU na Narc Kenya navyo vimejiunga na Muungano wa CORD katika harakati hizo za kuiondoa Tume ya IEBC.
Tayari Kamati ya Bunge inayosimamia maswala ya haki na sheria imewaalika makamishna wa tume ya uchaguzi kutafuta mwelekeo wa kukomesha mgogoro uliopo.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed abdul-Rahman