1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makao makuu ya serikali ya Somalia yavamiwa

Charo, Josephat8 Julai 2008

Wapiganaji wa kiislamu waliojihami na silaha nzito wameyavamia maeneo muhimu katika makao makuu ya serikali ya Somalia mjini Baidoa. Wanajeshi wasiopungua wanne wa Somalia wameuwawa katika uvamizi huo.

Wanajeshi wa Somalia wakishika doria katika barabara za BaidoaPicha: AP

Walioshuhudia uvamizi huo mjini Baidoa wanasema mabomu yaliyovurumishwa na wapiganaji wa kiislamu usiku wa kuamkia leo pia yaliulenga uwanja wa ndege na ghala lililofanyiwa marekebisho ambalo hutumiwa kama bunge la utawala unaoungwa mkono na nchi za magharibi.

Ibrahim Ali Isak, mlinzi katika ikulu ya rais iliyozungukwa na ukuta mrefu amesema waliangukiwa na mabomu hayo na wanajeshi watatu wakauwawa. Wanajeshi wengine saba walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini ambako kwa mujibu wa duru za maafisa wa hospitali hiyo, mwanajeshi mmoja alikufa kutokana na majeraha aliyoyapata.

Shambulizi hilo limefanywa na wapiganaji wa kundi la al-Shabaab ambalo Marekani imeliorodhesha kama kundi la kigaidi. Msemaji wa kundi hilo, Sheikh Mukhtar Robow, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa shabaha yao ilikuwa kuwashambulia walinzi wa rais wa Somalia na vikosi vya Ethiopia vinavyoisaidia serikali ya mpito ya Somalia.

Jeshi la kulinda amani

Waziri mkuu wa Somalia, Nur Hassan Hussein, amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa Ethiopia kwamba jumuiya ya kimataifa sharti ipeleke wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Somalia haraka iwezekanavyo, la sivyo usalama utaendelea kuzorota katika eneo la pembe ya Afrika. Aidha kiongozi huyo amesema vikosi vya Umoja wa Mataifa vinahitajika kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ethiopia kwa mujibu wa mkataba wa amani uliofikiwa na sehemu ya upinzani mwezi uliopita kwenye mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Djibouti.

Kundi la al Shabaab ni kitengo cha muungano wa mahakama za kiislamu uliotimuliwa kutoka mjini Mogadishu na wanajeshi wa serikali ya Somalia na wanajeshi wa Ethiopia mwanzoni mwa mwaka jana. Likiwa pamoja na wapinzani wenye misimamo mikali, kundi hilo limeukosoa mkataba wa Djibouti ambao haujafua dafu katika kukomesha umwagikaji wa damu unaoendelea nchini Somalia.

Mauaji

Muhanga wa hivi karibuni wa kundi hilo ni Osman Ali Ahmed, mkurugenzi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP nchini Somalia, aliyeuwawa Jumapili iliyopita na majambazi ambao mpaka sasa bado hawajajulikana. Mtoto wake wa kiume na kakake walijeruhiwa katika shambulizi hilo. Sheikh Mukhtar Robow amesema wanamgambo wa Al-Shabaab hawapaswi kulaumiwa kwa mauaji ya mkurugenzi huyo aliyepigwa risasi wakati alipokuwa akitoka msikitini.

Msemaji wa al-Shabaab, Sheikh Mukhtar Robow, ameyalaani vikali mauaji ya watu muhimu katika jamii ya wasomali na kusema kundi lake halikuhusika. Badala yake amewashutumu wanajeshi wa serikali ya Somalia na wa Ethiopia kwa mauaji ya mkurugenzi huyo. Maafisa wa serikali na jeshi la Ethiopia hawakuweza kufikiwa ili kujibu madai hayo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameuongoza ulimwengu katika kuyalaani mauaji ya Osman Ali Ahmed akiyaeleza kuwa kitendo cha kikatili kinacholenga kufuja juhudi za kibinadamu na amani nchini Somalia.

Marekani kupitia msemaji wa wizara ya ndani Sean McCormack pia imelaani vikali mauaji ya Osman Ali Ahmed.

Uvamizi wa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab dhidi ya makao makuu ya serikali ya Somalia unaonekana kutimiza ahadi yao ya kuendelea kupigana hadi wanajeshi wa Ethiopia waondoke Somalia, nchi ambayo imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu rais Siad Barre alipopinduliwa kutoka madarakani mnamo mwaka wa 1991.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW