Makocha wa Premier League waimarisha kikosi cha England
11 Juni 2018Katika kikosi cha kocha Gareth Southgate cha wachezaji 23 nchini Urusi, 15 walimaliza katika timu zilizoko katika nafasi nne za juu chini ya makocha nyota Guardiola, Klopp, Jose Mourinho na Mauricio Pochettino.
Manchester City imevunja rekodi kadhaa za Premier League wakati wakielekea katika ubingwa wao msimu huu, ambapo Raheem Sterling , Kyle Walker, John Stones na Fabian Delph wakionekana bila shaka yoyote wakiongeza viwango vyao chini ya kocha Pep Guardiola.
"Bila shaka," Delph aliliambia shirika la habari la AFP wakati alipoulizwa iwapo kocha wake kutoka jimbo la Catalonia alikuwa ufunguo wa kuchaguliwa kwake katika kikosi cha England. "Kwangu mimi ni mtu mwenye kipaji cha hali ya juu kabisa."
Mchezaji ambaye kawaida hucheza kama kiungo wa kati, Delph kwa muda mrefu wa msimu alichezea beki wa kushoto wakati Guardiola alitumia uwezo wake na kumpa majukumu mapya.
"Amefungua macho yangu kuona mambo mengi. Kuwahi kufikiria kuhusu kandanda kama Pep anavyofikiria," alisema Delph . "Kimsingi mimi ni Muingereza halisi. Naamini katika kufanya kazi ngumu na dhamira thabiti na kujitolea kwa kila kitu. Unafahamu kwamba niko hapa kupambana, kutafuta mipira inayorudi ya pili na kuwa mfano wa kizamani wa Mwingereza.
"Sasa inahusiana zaidi na kuwa mtulivu na kuwa makini unapokuwa na mpira."
Southgate anaamini Guardiola alikuwa anashawishi utaratibu wake wa kucheza kandanda kabla ya kuwasili nchini Uingereza, kutokana na kikosi chake cha ajabu cha Barcelona ambacho kilishinda mataji mawili ya Champions League katika muda wa miaka minne ya fahari kati ya mwaka 2008 na 2012.
Athari za Barcelona
"Athari zilizotokana na kuiona timu ya Barcelona miaka mitano hadi saba iliyopita ilikuwa kubwa," amesema Southgate. "Amekuwa mgunduzi. Wakati nikiangalia mpira wa watoto hii leo, wakati wakiingia katika viwnja ambavyo havikujaa maji ama kuganda barafu, nawaona wakicheza wakianzia nyuma.
"Siwaoni makocha vichwa vyao vikiwa katika mikono yao wakisema , "peleka mbele". Nafikiri hii ni athari ya timu yake, ikiwa na wachezaji kama Andres Iniesta na Xavi."
Hata hivyo , Guardiola sio kocha pekee ambaye ameisaidia England kufanya vizuri. Stones , Walker na Sterling walikuwa tayari wachezaji wa timu ya taifa kabla ya kupelekwa katika kiwango kingine na kocha huyo wa zamani wa Barca na Bayern Munich.
Kwa ulinganisho, Pochettino wa Tottenham amewaendelea wengi wa wachezaji nyota wa Southgate kama harry Kane na Dele Alli kutoka katika kiwango chao cha awali, na kuwabadilisha kutoka wachezaji ambao hawana majina kuwa wachezaji wenye majina makubwa. Danny Rose , Eric Dier na Kieran Trippier wanakamilisha kundi la wachezaji watano wa Spurs katika kikosi kilichoko nchini Urusi na wamekuwa wakisisitiziwa kucheza katika misingi ya udhibiti wa kandanda na kuweka mbinyo ambako Guardiola anahubiri kila mara.
Athari za Klopp
Trent Alexander-Arnold ameanza kuichezea kwa mara ya kwanza England katika ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Costa Rica baada ya kucheza vizuri katika msimu huu chini ya Klopp na kumalzikia katika fainali ya Champions League dhidi ya Real Madrid pamoja na nahodha wa Liverpool na mchezaji mwenzake katika kikosi cha England Jordan Henderson.
"Kama wachezaji wamepata fursa kubwa ya kucheza chini ya kocha kama huyo, kwasababu unajifunza mengi kutoka kwake," amesema Henderson, akimaanisha athari za Klopp.
Mourinho amewapa nidhamu ya ulinzi Ashley Young na kumbadilisha kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye hapo kabla alikuwa mshambuliaji wa pembeni na kuwa mlinzi wa kushoto ambaye kocha Southgate anamuona ni muhimu sana kwa kikosi chake kuliko Ryan Bertrand, ambaye amecheza mara tano katika duru za mchujo.
Na Jesse Lingard anatoa changamoto kwa dhana kwamba Mourinho hatoi nafasi kwa vijana na alifunga mabao 13 katika msimu wake mzuri kabisa akiwa na Manchester United na kutoa changamoto kwa kocha kumpanga katika kikosi cha kwanza katika mchezo wake wa ufunguzi dhidi ya Tunisia katika kundi G.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman