1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Makombora ya Urusi na mkururo wa droni vyaua wanne Kyiv

28 Septemba 2025

Urusi imerusha mamia ya makombora na droni dhidi ya Ukraine usiku kucha Jumapili, na kuua takribani watu wanne akiwemo msichana wa miaka 12 mjini Kyiv, huku majeruhi wakipindukia 40 katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Ukraine Kyiv 2025 | Shambulio la droni la Urusi likiangaza anga juu ya jiji
Ukraine imesema Israel ilitumia makombora na droni 500 katika mashambulizi ya usiku kucha dhidi ya Kyiv na miji mingine kote nchini humo.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Mashambulizi ya usiku kucha

Mamlaka za Ukraine zilisema mashambulizi hayo yalianza usiku wa Jumamosi na kudumu kwa takribani saa 12, yakilenga miji ya mashariki, kati na kusini mwa nchi.Zaidi ya makombora na droni 640 yalirushwa, hatua ambayo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliitaja kama "ugaidi wa vita.”

Katika mji mkuu, Kyiv, shabaha zilikuwa majengo ya makazi, ambapo msichana wa miaka 12 aliuawa pamoja na watu wengine watatu. Zaidi ya watu 40 walijeruhiwa katika mikoa ya Zaporizhzhia, Odesa, Sumy, Cherkasy na Mykolaiv.

Poland, jirani wa Ukraine na mwanachama wa NATO, ilipeleka ndege za kivita angani mara moja kulinda anga yake baada ya shambulio hilo, huku muungano huo wa ulinzi ukiishutumu Moscow kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa anga ya Ulaya Mashariki.

Zelensky alisema mashambulizi hayo yanaonyesha wazi kuwa Urusi "inataka kuendeleza vita na mauaji” na alisisitiza kuwa inastahili kukabiliwa na "shinikizo kali zaidi” kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Aliongeza kuwa serikali yake itajikita kudhoofisha uwezo wa Moscow kufadhili vita kupitia mapato ya nishati na kuilazimisha Urusi kukaa kwenye meza ya mazungumzo.

Waokoaji wakifanya kazi katika eneo la majengo ya ghorofa yaliyoharibiwa wakati wa shambulio la Urusi mjini Kyiv, Ukraine, Jumapili, Septemba 28, 2025.Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Mashuhuda wa mashambulizi

Kwa wakaazi wa Kyiv, mashambulizi hayo yalikuwa ya kutisha. Mark Sergeev, mwenye umri wa miaka 35, alisema familia yake ilikuwa imelala wakati kombora lilipogonga ghorofa yao katikati ya usiku. "Siamini kuwa watoto wako hai. Ni baraka ya Mungu. Paa lilichanika moja kwa moja juu ya kitanda cha mwanangu mkubwa,” aliliambia shirika la AFP.

Anna, 26, alisimulia jinsi nyumba yake ilivyoharibiwa na mlipuko. "Nilishtuka sana, sikusikia mengi. Nilihisi kishindo cha roketi kikiruka, kisha mlipuko na vioo vyote vikavunjika,” alisema.

Zelensky alichapisha picha zikionyesha majengo ya makazi yakiteketea kwa moto huku vikosi vya dharura vikihangaika kuzima moto na kuwaokoa manusura. Waliokoa kadhaa lakini wakaonya kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka baada ya ufukuaji wa vifusi kukamilika.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine, miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni kituo cha matibabu ya moyo na shule ya awali. Hali hii ilionyesha kuwa raia bado wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa mashambulizi ya Urusi.

Ripoti ya wanahabari wa shirika la AFP ilisema mashine nzito zilitumika kuondoa vifusi vya majengo yaliyokuwa karibu kuporomoka kabisa.

NATO na Poland zatuma onyo

Shambulio hili kubwa limekuja siku chache baada ya Urusi kuionya NATO kutochukua hatua kali zaidi kufuatia madai ya ukiukaji wa anga wa mara kwa mara. Hata hivyo, mataifa kadhaa ya Ulaya yamesema Urusi imekuwa ikitumia droni na ndege za kivita kujaribu azma ya muungano huo wa ulinzi.

Jeshi la Poland lilitangaza kwenye mtandao wa X kwamba lilituma ndege za kivita na kuweka mifumo yake ya ulinzi wa anga katika hali ya tahadhari ya juu.

Droni ya Urusi ikipaa juu ya jiji huku wanajeshi wa Ukraine wakifyatua risasi kuidungua wakati wa mashambulizi ya droni na makombora ya Urusi, dhidi ya Ukraine, mjini Kyiv, Ukraine, Septemba 28, 2025.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, akihutubia Umoja wa Mataifa mjini New York, alisema "shambulio lolote dhidi ya nchi yangu litajibiwa kwa hatua madhubuti.”

Urusi imeendelea kukanusha kwamba ina nia ya kushambulia taifa lolote mwanachama wa NATO, ikisema madai ya ukiukaji wa anga ni propaganda.

Lakini wachambuzi wanasema misururu hii ya mashambulizi inalenga kuwatisha washirika wa Ukraine na kuonyesha udhaifu wa ulinzi wa anga wa muungano huo.

Silaha mpya na hofu ya nyuklia

Zelensky alisema nchi yake sasa imepokea mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot kutoka Israel na inatarajia mifumo mingine miwili hivi karibuni. Alieleza kuwa msaada huo wa kijeshi ni muhimu kuimarisha ulinzi wa anga wakati mashambulizi ya Urusi yakiongezeka.

Msimamo wa Israel umebadilika kwa kiasi kikubwa, baada ya uhusiano wake na Moscow kudhoofika kutokana na urafiki wa karibu wa Urusi na Iran na msimamo wake kuhusu vita vya Gaza.

Wakati huo huo, kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia kilichopo chini ya udhibiti wa Urusi, na ambacho ndicho kikubwa zaidi barani Ulaya, kimeripotiwa kimeondolewa kwenye gridi ya taifa kwa siku nne mfululizo. Taarifa hiyo imezidisha hofu ya tukio la hatari la nyuklia.

Wachambuzi wanaonya kuwa hali hii inazidisha hatari ya ajali kubwa inayoweza kuathiri sio Ukraine pekee bali pia nchi jirani za Ulaya.

Kwa sasa, juhudi za kidiplomasia kurejesha amani zimekwama, huku Moscow ikisisitiza kuwa haitaacha mashambulizi yake.

NATO ni nini?

02:15

This browser does not support the video element.

Mustakabali wenye wasiwasi

Vita hii, ambayo sasa inaelekea kuingia mwaka wa nne, inazidi kukomaza misimamo ya pande zote. Ukraine inategemea msaada wa kijeshi na kifedha kutoka kwa washirika wake, huku Urusi ikiendelea kunufaika na mauzo ya nishati.

Wataalamu wanasema mzozo huu unaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi, bila shinikizo kuongezwa dhidi ya Moscow kushiriki mazungumzo.

Kwa raia wa Ukraine, mashambulizi ya kila siku yamekuwa sehemu ya maisha, lakini simulizi za manusura zinaonyesha machungu ya kijamii na kiakili yanayozidi kuongezeka.

Kwa dunia nzima, mashambulizi haya yanaongeza wingu la hofu la kusambaa kwa mzozo na kuathiri usalama wa kikanda na kimataifa.

Ukraine inasema itaendelea kupigana hadi haki ipatikane, huku ikisisitiza kuwa lengo lake ni kulazimisha Urusi kwenye meza ya mazungumzo.

Chanzo:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW