1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya Urusi yashambulia Odesa

21 Juni 2022

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa makombora yake yameushambulia uwanja wa ndege karibu na mji wa bandari wa Odesa nchini Ukraine.

Nächtliche Luftangriffe an Odesa
Picha: Oleksandr Gimanov/AFP

Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Urusi, vikosi vya nchi hiyo vimefanya mashambulizi katika kujibu shambulizi la Ukraine kwenye eneo la kuchimba gesi kwenye Bahari Nyeusi.

Kiongozi wa Crimea aliyewekwa na Urusi, katika rasi hiyo ya Ukraine ambayo ilinyakuliwa na Urusi mwaka 2014, amesema Kiev ilifanya shambulizi katika maeneo ya kuchimba gesi kwenye Bahari Nyeusi ambayo yanamilikiwa na kampuni ya mafuta ya Crimea. Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha taarifa hizo.

Hayo yanajiri wakati ambapo Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Merrick Garland leo anaizuru Ukraine kujadiliana kuhusu mashtaka ya watu waliohusika na uhalifu wa kivita katika taifa hilo la Ulaya lililovamiwa na Urusi mwishoni mwa mwezi Februari.

Wizara ya Sheria ya Marekani imesema kuwa Garland atakutana na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine, Iryna Venediktova, karibu na mpaka wa Poland na Ukraine.

Maafisa hao watajadiliana kuhusu juhudi za Marekani na kimataifa kuisaidia Ukraine, kuwatambua, kuwakamata na kuwashitaki watu waliohusika na uhalifu wa kivita na ukatili mwingine nchini Ukraine. Garland anaizuru Ukraine, akiwa njiani kuelekea mjini Paris, Ufaransa kuhudhuria mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Marekani na Umoja wa Ulaya.

Shehena ya kwanza ya makombora kutoka Ujerumani imepelekwa Ukraine

Picha: Frank Hofmann/DW

Wakati huo huo, Ukraine imesema kuwa hatimaye shehena ya kwanza ya mfumo wa kisasa wa kuzuia makombora wa Ujerumani umepelekwa Ukraine. Hizo ni silaha za masafa marefu ambazo Ukraine imekuwa ikiziomba kutoka katika nchi za Magharibi.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba mfumo wa makombora aina ya PzH 2000 ni sehemu ya ushirikiano wa jumuia ya kimataifa katika kuisaidia Ukraine. Reznikov alikuwa akimshukuru Waziri mwenzake wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht.

Ama kwa upande mwingine, Lithuania imekataa shinikizo la Urusi kuhusu kuondoa vizuizi katika usafiri wa reli kwenda na kutoka eneo la Urusi la Kaliningrad. Waziri Mkuu wa Lithuania, Ingrida Simonyte amesema leo kuwa hakuna kizuizi katika eneo hilo.

''Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita vikwazo vimewekwa kwenye baadhi ya bidhaa ikiwemo kile kinachojulikana kama kifurushi cha vikwazo, yaani chuma. Usafirishaji wa bidhaa nyingine zote ambazo ama hazijawekewea vikwazo unafanyika pamoja na usafiri wa abiria chini ya makubaliano maalum kati ya Umoja wa Ulaya, Urusi na Lithuania,'' alifafanua Simonyte.

Nayo mataifa ya Baltic yametoa wito wa kupewa msaada zaidi wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuzisaidia kukabiliana na wimbi la wakimbizi wa Ukraine wanaoingia kwenye nchi hizo.

(AFP, DPA, AP, Reuters, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW