1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano bado kitendawili mazungumzo ya Vienna

23 Novemba 2014

Iran na mataifa yenye nguvu duniani wanakabiliwa na kazi ngumu leo Jumapili(23.11.2014) kuvunja mkwamo katika majadiliano yao muhimu ya kinyuklia na kupata makubaliano ya kihistoria kabla ya muda wa mwisho kumalizika.

Iran Atomgespräche 21.11.2014 Wien
Majadiliano katika meza ya duara mjini Vienna 21.11.2014Picha: Reuters/Heinz-Peter Bader

"Tunafanyakazi kwa nguvu," waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema jana Jumamosi (22.11.2014) mjini Vienna, "na tunamatumaini tunapiga hatua, lakini tuna mianya mikubwa, bado tuna mianya mikubwa, ambayo tunaifanyia kazi kuiziba."

Kerry , ambaye siku ya Ijumaa aliahirisha safari yake mjini Paris ili kubakia mjini Vienna kwa mazungumzo hayo, amekutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif mchana jana Jumamosi, ukiwa mkutano wao wa nne katika siku tatu.

waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Steinmeier (kushoto) na John Kerry wa Marekani (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/H. Punz

Makubaliano ni lazima

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier , pia akiwa mjini Vienna , amesema hili ni mwisho wa juma la mwisho la mazungumzo, baada ya miezi kadhaa ya majadiliano, wakati "wa ukweli".

Kunatakiwa kupatikana makubaliano ya kihistoria ambapo Iran inazuwia shughuli zake zinazobishaniwa za kinyuklia ili ipate afueni kubwa ya miaka kadhaa ya vikwazo vya kimataifa vya kiuchumi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad ZarifPicha: picture-alliance/dpa

Makubaliano hayo yanaweza kufikisha mwisho mkwamo wa miaka 12 ambao ulileta uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya vinu vya kinyuklia vya Iran. Kerry amezungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumamosi kwa simu.

"Mwanya unabaki kubwa mkubwa...Kwa sasa kunahitajika uamuzi wa kisiasa, " duru kutoka Iran imeliambia shirika la habari la AFP kwa masharti ya kutotajwa jina, na kuweka jukumu kwa mataifa yenye nguvu duniani kufanya maridhio.

Wajumbe wa majadiliano wa Iran wamesifiwa na maafisa nchini Iran kwa kuheshimu misingi ya nchi yao."

Nafasi ni finyu ya kupatikana makubaliano

Duru za mataifa ya Ulaya katika mazungumzo hayo zimesema , "hakuna hatua muhimu zilizopigwa" na " nafasi ya kupatikana makubaliano iko chini mno".

"Ili kupatikana makubaliano Wairani ni lazima kutoa maridhio katika hali ya juu," amesema.

Majadiliano juu ya kurefusha muda wa majadiliano yanaweza kuanza mapema leo Jumapili(23.11.2014), chanzo hicho kimesema.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/AP Photo

Wataalamu wengi wanaamini kwamba muda wa mwisho utarefushwa, kama ilivyotokea mapema Julai 20 mwaka huu, lakini maafisa wanasisisitiza kwamba hilo bado halijafikishwa mezani kwa majadiliano bado.

Hata hivyo, afisa mwandamizi wa Marekani amesema baadaye jana Jumamosi kwamba lengo linabakia kupata makubaliano ifikapo Jumatatu usiku " lakini tunajadiliana ndani pamoja na washirika wetu kuhusu uwezekano kadhaa.

Maandamano yalifanyika mjini Vienna kupinga mpango wa Iran wa kinyuklia.Picha: Reuters/H.-P. Bader

Marekani , Urusi , China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimekuwa zikifanya majadiliano na Iran tangu Februari mwaka huu kubadilisha makubaliano ya mpito yaliyofikiwa mwaka mmoja uliopita kuwa makubaliano ya kudumu ifikapo Novemba 24.

Makubaliano kama hayo yana lengo la kupunguza hofu kwamba Tehran inatengeneza silaha za kinyuklia chini ya kivuli cha shughuli za kiraia za kujipatia nishati.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afp