1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano kati ya Israel na Hamas yaendelea kuheshimiwa

20 Januari 2025

Makubaliano tete ya usitishaji vita Gaza kati ya Israel na Hamas yameendelea kuheshimiwa leo baada ya Jumapili kushuhudiwa mpango wa kubadilishana wafungwa 90 Wakipalestina na mateka watatu raia wa Israel.

Watu wazingira basi lililowabeba wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru kutoka gereza la Israel karibu na Ramallah mnamo Januari 20,2025
Watu wazingira basi lililowabeba wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru kutoka gereza la IsraelPicha: Ammar Awad/REUTERS

Vyombo vya habari vya ndani, ikiwa ni pamoja na gazeti la mtandaoni la The Times la Israel, vilinukuu mamlaka ya gereza hilo ikithibitisha kuachiliwa kwa wafungwa hao na kusema wengi wao walikuwa wanawake na watoto.

Kulingana na ripoti hizo, wafungwa wengi wanatoka Ukingo wa Magharibi, huku wengine wakitoka eneo la Jerusalem Mashariki.

Usitishaji mapigano waanza kutekelezwa Gaza

Vyombo vya habari vya Palestina vilionyesha kanda za video na picha za kile walichosema ni wafungwa waliokuwa wakiwasili Ramallah.

Hapo jana, kundi la hamas, liliwaachilia huru mateka watatu wa kwanza wa Israel kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Matekwa wa Israel walioachiliwa huru

Wanawake hao watatu waliotajwa na jeshi la Israel kama Romi Gonen, Emily Damari na Doron Steinbrecher, walikabidhiwa na kundi hilo la wanamgambo kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) jana alasiri.

Malori ya misaada yaanza kuingia Gaza

Baadaye, walipokewa na vikosi vya Israeli na kusafirishwa hadi katika hospitali  moja huko Tel Aviv, ambapo walilakiwa na familia zao.

Mateka wa Israel Romi Gonen akumbatiwa na baada ya kuachiliwa huru na kundi la Hamas Picha: Israel Defense Forces/Handout/REUTERS

Msemaji wa kundi la Hamas alithibitisha kuwa mateka wanne zaidi wa Israel wataachiliwa huru siku ya Jumamosi, kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana mateka 33 kwa wafungwa 1,904 wa Kipalestina ambao wanazuiliwa kwenye jela za Israel kwa kipindi cha wiki sita.

China yapongeza makubaliano kati ya Israel na Gaza

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning, amesema nchi yake inapongeza kuanza kutekelezwa kwa makubaliano hayo ya kusitishwa kwa mapigano.

Ning ameongeza kuwa wanatumai makubaliano hayo yatatekelezwa kikamilifu na mfululizo na kwamba usitishajiwa kudumu wa vita huko Gaza utafikiwa.

Kihistoria, China imekuwa ikiunga mkono mchakato wa Palestina wa suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo huo kati ya Israel na Palestina.

Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina wakamatwa mjini Berlin

Watu kadhaa wamekamatwa katika maandamano ya kuiunga mkono Palestina mjini Berlin, yaliofanywa saa chache baada ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya amani kati ya Israelna kundi la wanamgambo la Hamas hapo jana ili kusitisha vita katika ukanda wa Gaza.

Katika ujumbe uliochapishwa na polisi katika mtandao wa kijamii wa X jana jioni, washiriki wa maandamano hayo walikuwa wakitoa kauli zilizopigwa marufuku dhidi ya Wayahudi, na kuongeza kuwa watu 12 walikamatwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW