Makubaliano kuzima mzozo wa Lebanon
16 Mei 2008Makundi yanayozozana nchini Lebanon yamekubaliana hapo jana juu ya makubaliano ya usuluhishi chini ya Jumuiya ya Waarabu kuanza mazungumzo ya kuzima mfarakano wa muda mrefu ambao umeiweka nchi hiyo iliogawika sana kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Chini ya makubaliano hayo yaliotangazwa baada ya siku mbili za mazungumzo mazito makundi hayo yamekubali kuanzisha tena mazungumzo ya kukomesha mzozo wa kisiasa unaoidhoofisha nchi hiyo ambao ulikuja kuzusha mapambano ya madhehebu ya siku sita yaliosababisha maafa wiki iliopita.
Viongozi wa Kiarabu wamekuwa mbioni kukomesha mzozo huo kati ya serikali ya Lebanon inayoungwa mkono na Marekani na upinzani unaongozwa na Hezbollah mzozo ambao kwa jumla unaonekana kuwa kati ya washirika wa Marekani huko Mashariki ya Kati na maadui zao wa Syria na Iran.
Chini ya mpango huo wa vipengele sita uliotangazwa na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jaseem al- Thani mahasimu hao wamekubali kwenda Qatar leo hii kuanza mazungumzo ya kitaifa kujaribu kumchaguwa rais na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Katika changamoto kubwa kabisa kuwahi kukabiliwa na Waziri Mkuu Fuad Siniora wapiganaji kutoka upinzani unaoungwa mkono na Iran walipambana na wapiganaji wanaounga mkono serikali wiki iliopita na kutwaa sehemu kubwa ya magharibi mwa Beirut katika umwagaji mbaya kabisa wa damu wa madhehebu kuwahi kushuhudiwa tokea vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi mwaka 1990.
Chini ya makubaliano hayo ya jana mahasimu hao wamekubaliana kuanzisha upya mazungumzo ya kuipa nguvu serikali ya taifa la Lebenon nchini kote,kuepuka kutumia silaha kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa na kuwaondowa wanamgambo wenye silaha mitaani.
Makubaliano hayo pia yanataka kuondolewa kwa vizuzi vya barabarani ambavyo vimezuia usafiri wa anga na kufunga barabara kuu na kwa mahasimu wao kujiepeusha kutumia lugha ambayo inaweza kuchochea vurugu.
Baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo wanamgambo walio tiifu kwa Hezbollah walianza kuondowa vikwazo kwenye barabara kuu ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut na kuruhusu kuanza tena kwa safari za ndege za kibiashara.
Matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano hayo yaliongezeka baada ya serikali kuregeza msimamo hapo Jumatano kwa kufuta hatua zilizozusha utata dhidi ya Hezbollah ambazo zimechochea machafuko ya hivi karibuni kabisa ambayo yameuwa takriban watu 65 na kujeruhi wengine 200.
Ilibatilisha mpango wa kuchunguza mtandao wa mawasiliano wa Hezbollah na kumpangia kazi mpya mkuu wa usalama uwanja wa ndege kutokana na madai kwamba ni mtu alie karibu na kundi hilo la wanamgambo wa madhehebu ya Shia hatua ambayo kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrullah ameita kuwa ni tangazo la vita.
Wachambuzi wa mambo wameonya kwamba kubadili huko msimamo kwa serikali dhidi ya kundi la Hezbollah kumedhoofisha serikali ya Siniora katika mzozo wake na upinzani na ni idhara kwa mshirika wake wa Marekani ambapo ni hapo jana tu Rais George Bush wa Marekani akiwa nchini Israel amehakikisha tena kuiunga mkono kikamilifu serikali hiyo.
Bush amesema kile kilichotokea Lebanon ni kwamba Hezbollah inayojulikana kama ndio mlinzi wa Walebanon dhidi ya Israel sasa imewageukia watu wake wenyewe. Hezbollah inaungwa mkono na Iran na hizi ni juhudi za Iran kudhoofisha demokrasia changa ya taifa hilo.Marekani itasimama kidete na serikali ya Siniora.
Bunge la Lebanon linatarajiwa kuitishwa tena Juni 10 katika jaribio lake la 20 kumchaguwa Rais wa kuchukuwa nafasi a kibaraka wa Syria Emin Lahoud alien'gatuka baada ya kumalizika kwa muda wake hapo mwezi wa Novemba.
Pande zote zimekubali mkuu wa majeshi Michel Sleiman ashike wadhifa huo lakini zinazozana juu ya muundo wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa na sheria mpya kwa ajili ya uchaguzi wa bunge unaotazamiwa kufanyika hapo mwakani.