1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano mapya yatangazwa Nagorno-Karabakh

26 Oktoba 2020

Armenia na Azerbaijan zimesisitiza dhamira yao ya kutafuta suluhisho la amani kwa mgogoro huo uliodumu miongo kadhaa na kukubali kujaribu kwa mara ya tatu kutekeleza mpango wa kuweka chini silaha 

Aserbaidschan-Armenien | Konflikt in Berg-Karabach
Picha: Julia Hahn/DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalioanza kutekelezwa leo saa mbili asubuhi yalitangazwa katika taarifa ya pamoja na serikali za Marekani, Armenia na Azerbaijan. Mikataba miwili ya awali ya kusitisha mapigano iliyosimamiwa na Urusi, ukiwemo mmoja wa mwishoni mwa wiki iliyopita, ilivunjika mara tu baada ya kuanza kutekelezwa, huku pande zote zikilaumiana kwa ukiukaji wake. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema jana usiku kuwa Marekani ilifanikisha mazungumzo makali na kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Armenia Zohrab Mnatsakanyan na mwenzake wa Azerbaijan Jeyhun Bayramov wamekubali kuanza kuutekeleza mpango huo leo. Na wakati Pompeo alikuwa akifanya mazungumzo tofauti na mawaziri hao, mapigano yalikuwa yamepamba moto Nagorno-Karabakh

Waziri Pompeo mwenzake wa Azerbaijan BayramovPicha: Hannah McKay/Reuters

Urusi, Marekani na Ufaransa, wenyekiti wenza wa kile kinachofahamika kama Kundi la Minsk lililoundwa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya kuusuluhisha mzozo huo, pia zilishiriki katika mazungumzo hayo. Soma zaidi: Armenia, Azerbaijan zalaumiana kukiuka makubaliano ya amani

Katika taarifa tofauti, wenyekiti wenza wa kundi hilo walisema watakutana na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Armenia na Azerbaijan mjini Geneva Alhamisi wiki hii, kujadili, kufikia makubaliano, na kuanza utekelezaki wa hatua zote mwafaka za kufanikisha suluhisho la amani katika mzozo wa Nagorno-Karabakh.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyakaribisha makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na kusisitiza ombi lake kwa Armenia na Azerbaijan kuyatekeleza kikamilifu bila kuchelewa na kuendelea na mazungumzo bila masharti ya kabla.

Waziri Pompeo na mwenzake wa Armenia MnatsakanyanPicha: Hannah McKay/Reuters

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote kuruhusu uingizwaji wa misaada ya kiutu katika jimbo la Nagorno-Karabakh. Kwa mujibu wa maafisa wa mkoa huo, wanajeshi wao 974 na raia 37 wameuawa katika makabiliano hayo mpaka sasa. Maafisa wa Azerbaijan hawajafichua hasara iliyotokea kwa jeshi lao, lakini wanasema mapigano yameuwa raia 65 na kuwajeruhi 300.

Wiki nne za mapigano zimezusha wasiwasi wa mgogoro mpana unaohusisha Uturuki, ambayo imetangaza kuiunga mkono Azerbaijan, na Urusi ambayo ina mkataba wa usalama na Armenia. Soma zaidi: Mzozo wa Nagorno-Karabakh unazidi kufukuta

Pia umeipa wasiwasi Iran, ambayo inapakana na Armenia na Azerbaijan. Jeshi la Mapinduzi la Iran jana lilipeleleka vikosi vyake vya ardhini kwenye mpaka karibu na eneo la mzozo.

Mwandishi: Bruce Amani
AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW