1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani kutiwa saini Jumatatu?

10 Novemba 2013

Waasi wa kundi la M23 na serikali ya Kongo wanatarajiwa kutia saini makualiano ya amani tarehe 11.11.2013 mjini Kampala wiki moja baada ya M23 kutangaza kusalimu amri vitani

Kamanda mkuu wa jeshi la wapiganaji wa M23 Brigedia Jenerali Sultani Makenga
Kamanda mkuu wa jeshi la wapiganaji wa M23 Brigedia Jenerali Sultani MakengaPicha: MICHELE SIBILONI/AFP/Getty Images

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la maziwa makuu Mary Robinson amesema kwamba makubaliano ya amani yanayosubiri kutiwa saini kesho Jumatatu na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kundi la waasi la M23 ni hatuwa muhimu kwa ajili ya amani katika kanda hiyo.

Halikadhalika mjumbe huyo ameapa kwamba jeshi la taifa na kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa chenye mamlaka ya kuingilia kati vita hivyo vitaendelea kwa pamoja kushirikiana katika juhudi za kuyamaliza makundi mengine ya waasi mashariki ya Kongo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu maziwa makuu Mary RobinsonPicha: AP

''Kuna mitazamo tofauti juu ya kinachofanywa na serikali na Monusco kwa pamoja mashariki ya Kongo lakini sasa makundi yote ya waasi yatashughulikiwa'' amesema mjumbe huyo ambaye ni rais wa zamani wa Ireland.

Kundi la waasi la M23,mojawapo ya makundi yenye silaha yanayoendesha operesheni zao katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini lakini masikini kabisa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo limepata pigo kubwa na hatimae kusalimu amri baada ya kukabiliwa na jeshi la taifa likiungwa mkono na kikosi maalum cha Monusco.Kundi hilo la M23 linatarajiwa kutia saini makubaliano ya amani mjini Kampala nchini Uganda Jumatatu mkataba ambao unaiweka katika mchakato rasmi ahadi yao ya kuachana na uasi wa miazi 18 pamoja na kulivunja kundi hilo.

Pongezi kwa Jeshi

Bibi Robinson amelipongeza jeshi la Kongo akisema ni jambo la kutia moyo kuona jeshi la Kongo FARDC likipata ushindi dhidi ya kundi la waasi na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu kama jeshi la taifa.Halikadhalika mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema ni kitu kizuri kwamba mchakato wa Kampala unafikia mwisho wake kwa kutiwa saini kwasababu kuna maelewano juu ya kuwajumuisha wapiganaji wa M23 katika jeshi la taifa au alau kuwaruhusu kurejea nyumbani.Ama kwa upande mwingine ameyataja mafanikio hayo pamoja na kutiwa saini makubaliano ya Kampala siku ya Jumatatu ni hatua zitakazofikisha mwisho madhila na mateso ya muda mrefu kwa raia wa jimbo la Kivu.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Joseph Kabila katika mkutanowa PretoriaPicha: picture-alliance/dpa

Kipaombele

''Umekuwa muda mrefu wa mateso yasiokubalika na sasa kuna matumaini ya kweli'' amesema bibi Robinson.Kitakachopewa kipaombele nchini Kongo kwa mujibu wa bibi Robinson ni mapambano sasa dhidi ya waasi Wakihutu kutoka Rwanda waliokita kambi nchini Kongo FDLR,kundi ambalo ni sehemu ya wapiganaji wa Kihutu wenye msimamo mkali waliohusika katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda.Serikali ya Rwanda inayoongozwa na kabila la Watutsi walio wachache inalitazama kundi hilo la FDLR kama kitisho kikubwa cha usalama kwa taifa lake na imekuwa ikituhumiwa na Umoja wa Mataifa kuhusika katika kuwaunga mkono waasi wa M23.Mary Robinson amezungumzia suala hilo akitowa kauli ya kutaka kishughulikiwe kiini cha kuzuka makundi haya.

''Nadhani imetambulika kwamba kuna haja ya kushughulikia sababu za ndani,kwa kuwa kiini cha kuibuka kundi la waasi la M23 ni kilio cha kweli cha Watutsi ambao hawajihisi kuwa nyumbani ndani ya nchi yao wenyewe na hapa tunazungumzia Kongo''

Mwandishi:Saumu Mwasimba/Afp

Mhariri:Mohammed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW