Makubaliano ya amani Ukraine yanaweza kufikiwa karibuni
2 Januari 2023Mchambuzi huyo Hans-Lothar Domröse ametabiri kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano kati ya Urusi na Ukraine hata kabla ya katikati ya mwaka huu.
"Natarajia katika majira ya joto, wakati pande zote zitakaposema, hili haliendi kokote, " Hans-Lothar Domröse alikiambia gazeti la Ujerumani la Funke.
Amesema kutashuhudiwa mkwamo kati ya mwezi Februari na Mei, na wakati huo ndipo mazungumzo ya kusitisha mapigano yatakapoanza.
Soma Zaidi:Urusi yazidisha mashambulizi nchini Ukraine kwa lengo la kutwaa tena miji iliyoipoteza
Hata hivyo amesisitiza kwamba hatua hiyo haimaanishi kwamba kumefikia amani. "Usitishwaji wa mapigano hakumaanishi kwamba mapigano ndio yamemalizika. Makubaliano yanaweza kuchukua muda mrefu, unahitaji msuluhishi," alisema, akiwataja katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ama rais wa India Narendra Modi, kama watu wanaofaa kuongoza mchakato wa usuluhishi.
Amesema, jambo moja linalosalia hapa ni suluhu ya makubaliano izakayokubaliwa na pande zote, "hata kama Vladimir Putin pengine atakuwa anapenda kuichukua Ukraine yote, Volodymyr Zelenskiy kwa upande wake atataka kuikomboa tena nchi yake yote."
Soma Zaidi:Kansela Scholz ahimiza mshikamano kuelekea mwaka mpya 2023
Mtaalamu wa mambo kuhusu Urusi na Ukraine András Rácz katika Baraza la Ujerumani, linalojishughulisha na masuala ya mahusiano ya kimataifa naye anaamini kutakuwepo na uwezekano wa kufikiwa na makubaliano katik ya Ukraine na Urusi kwenye majira ya joto ya mwaka huu.
"Nina uhakikika kwamba ifikapo mwishoni mwa mwaka tutakuwa na aina fulani ya usitishwaji wa mapigano: tukiwa na matumaini ya kutokuwepo na mapigano kabisa, ama labda mapigano kiasi," Rácz aliliambia gazeti hilo.
Amesema, hakuna uwezekano kwamba Urusi ingetaka kuanzisha vita vikali hata kabla au wakati wa uchaguzi wa urais unaopaswa kufanyika mwaka wa 2024. Kwa maana hiyo anatarajia Urusi itataka kupunguza makali ya mapigano katika kipindi cha 2023. "Hii pia ni kwa sababu huenda Urusi ikakabiliwa na kuongezeka kwa changamoto za wanajeshi," Rácz aliongeza.
Mwenyekiti wa kamati ya mahusiano ya kigeni kwenye Bunge la Ulaya, David McAllister amesisitiza kwamba ikulu ya Urusi, Kremlin isingeweza na haitakiwi kuleta ubabe katika mchakato wa amani na Ukraine.
"Iwapo na wakati kutatolewa masharti ya kusitishwa mapigano, ni serikali ya Ukraine pekee ndio itatakiwa kuamua," McAllister aliliambia gazeti la Funke