Makubaliano ya biashara yafikiwa duniani
7 Desemba 2013Waziri wa biashara wa Indonesia Gita Wirjawan amesema baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo katika siku ya tano ya mazungumzo kwenye kisiwa hicho cha Indonesia kwamba ni kwa kupitia tu makubaliano ya kimataifa nchi nyingi za kimaskini na zile ziliokuwa rahisi kuathirika zinaweza kufaidikia hasa na biashara ya kimataifa.Waziri huyo amesema " hongera sio tu kwa kuiweka hai Agenda ya Maendeleo ya Doha bali kuwapa nguvu mpya na imani mpya ya kukamilisha mazungumzo hayo ya kibiashara ya Duru ya Doha."
Kile kinachojulikana kama mpango wa Bali ni mkataba wa kwanza wa biashara wa kimataifa ambao umeweza kufanikishwa na nchi wanacahama 159 wa WTO baada ya mazungumzo ya takriban miaka 20.Unakusudia kupunguza vikwazo vya urasimu vyenye kukwamisha biashara na pia unajumisha hatua za kuzisaidia nchi za kimaskini kuingia kwenye masoko ya nchi zilizoendelea na zile zinazoinukia kiuchumi pamoja na hatua nyengine za misaada.
Uchumi wa dunia kunufaika
Makubaliano hayo pia yanahusisha hatua za kurahisisha biashara kwa kuregeza taratibu za forodha na upunguzaji wa ruzuku za kilimo. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema katika taarifa kwamba makubaliano hayo yatakuwa kichocheo hasa na uwezekano wa faida kwa uchumi wa dunia inaweza kufikia hadi dola trilioni moja.
Amesema makubaliano hayo yatatowa msaada muhimu kwa watu maskini duniani kote katika nchi zenye maendeleo duni duniani. Ameongeza kusema " WTO imerudi tena kwenye mkondo na kufanikisha mageuzi". Umoja wa Ulaya utatowa euro milioni 400 katika kipindi cha miaka mitano kuzisaidia nchi zinazoendelea ambapo Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya Karel De Gucht akisema kwamba uwekezaji huo utaleta faida kubwa linapokuja suala la ukuaji wa uchumi,ajira na maendeleo.Kwa mujibu wa Gucht makubaliano hayo pia yatazisaidia nchi zinazoendelea kuokowa takriban euro 325 milioni kwa mwaka.
Duru ya Doha yakwamuliwa
Mawaziri wa biashara pia wameelezea matokeo ya kufanikiwa kwa mazungumzo hayo yamesaidia kukwamua mazungumzo yaliokwama ya Duru ya Doha ambayo yalianza mwaka 2001 na agenda ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kutekeleza sheria za biashara huru za Shirika la Biashara Duniani WTO. Makubaliano rasmi ya rasimu ya mazungumzo hayo yalicheleweshwa hapo Jumamosi kutokana na Cuba kusisitiza kwa masaa kadhaa kwamba vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vya miongo mitano dhidi ya nchi hiyo ya Kikomunisti ya Caribean viondolewe.
Lakini kikwazo kikuu zaidi katika mazungumzo hayo kiliondolewa hapo Ijumaa wakati wajumbe walipoweza kupata ufumbuzi kwa madai ya India ya kutaka iruhusiwe kutowa ruzuku kwa bidhaa za kilimo ili kuweza kuwalisha watu maskini.Chini ya makubaliano yalioafikiwa,India haitoruhusiwa kuendelea na sera hiyo milele bali ni kwa miaka minne tu.India pia inatakiwa ihakikishe kwamba bidhaa zake haziishii kusafirishwa kwenye masoko mengine ambapo zinaweza kusababisha kushuka kwa bei.
WTO yafana
"Kwa mara ya kwanza katika historia yetu WTO imewasilisha hasa kile kinachotakiwa",amesema hayo Mkurugenzi wa shirika hilo la biashara duniani Roberto Azevedo.Makubaliano hayo yanaonekana kama ushindi binafsi kwa Azevedo raia wa Brazil ambaye ameshika wadhifa huo hapo mwezi wa Septemba na kuingiza hisia ya dharura katika mazungumzo hayo.
Viongozi katika mkutano huo wamesisitiza kwamba makubaliano hayo ya Bali ni muhimu katika kuhakikisha kwamba shirika la WTO linaendelea kuwa na maana licha ya juhudi za hivi karibuni za Marekani,Umoja wa Ulaya, China na wengineo kuwa na makubaliano ya kibiashara ya kikanda badala ya yale ya dunia.
Mkutano huo pia umeikubali rasmi Yemen kuwa mwanachama wa 160 wa shirika hilo na bunge la Yemen lina muda wa miezi sita kuridhia kujiunga na shirika hilo.
Mwandishi:Mohamed Dahman/dpa/AFP/
Mhariri : Abdu Mtullya