Makubaliano ya kusitisha vita Iran, Marekani mashakani
9 Aprili 2026
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran alisema nchi yake ingeliziruhusu meli kupita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz kwa mujibu wa "sheria na kanuni za kimataifa" mara tu "Marekani itakapoacha uchokozi" wake kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati na Israel nayo kuacha kuishambulia Lebanon.
Akizungumza na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) siku ya Alkhamis (Aprili 9), Saeed Khatibzadeh, alisema Iran iliufunga tena Mlango Bahari huo baada ya mshirika wa Marekani, Israel, kuyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano siku ya Jumatano (Aprili 8) kwa kuishambulia Lebanon.
"Huwezi kuila keki yako na kisha ukabakia kuwa nayo kwa wakati mmoja. Huo ndio ujumbe ambao Iran imeutuma kwa uwazi na ufasaha kabisa kwa Washington na kwa Ikulu ya Marekani usiku wa jana," alisema Khatibzadeh.
Kwa mujibu wa utawala wa Marekani, kuufunguwa Mlango Bahari wa Hormuz bila masharti yoyote ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa usiku wa kuamkia Jumatano.
Lakini Tehran inasema mpango wa vipengele 10 iliouwasilisha na kukubaliwa na Washington unataja waziwazi kuwa Mlango Bahari huo utaendelea kuwa kwenye udhibiti wake na pia usitishwaji mapigano unazihusisha pia Lebanon, Iraq, Yemen na Palestina.
Pakistan yaendelea na matayarisho ya mazungumzo
Wakati huo huo, serikali ya Pakistan ilikuwa ikiendelea na matayarisho ya mwisho mwisho ya mkutano wa kwanza wa moja kwa moja kati ya wajumbe wa Marekani na Iran uliotazamiwa kuanza Ijumaa (Aprili 10).
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, , alikutana siku ya Alkhamis na Mwambata wa Ubalozi wa Marekani, Natalie Baker, kujadiliana hali ilivyo Mashariki ya Kati na mazungumzo hayo ya Ijumaa.
Taarifa rasmi ya serikali ya Pakistan iliwataja miongoni mwa wajumbe wa Marekani kuwa ni Makamu wa Rais JD Vance, mjumbe maalum wa Rais Trump, Steve Witkoff, na mkwe wa Trump, Jared Kushner.
Lakini Balozi wa Iran nchini Pakistan, Reza Amiri Moghadam, aliufuta ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao ulikuwa umesema wajumbe kutoka Tehran kwa ajili ya mazungumzo hayo wangewasili usiku wa Alkhamis.
Haijafahamika ikiwa Iran ingelituma wajumbe wake hao au ingelitimiza onyo lake la Jumatano kwamba "bila ya kusitishwa mashambulizi dhidi ya washirika" wake, ingelilazimika kujiondowa kwenye makubaliano ya usitishaji mapigano.
Arubaini ya Khamenei
Kwenyewe nchini Iran, maelfu ya waombolezaji walikusanyika siku ya Alkhamis katika mji mkuu Tehran kuomboleza katika siku ya 40 tangu kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wao mkuu, Ayatullah Ali Khamenei, siku ya mwanzo kabisa ya mashambulizi ya Israel na Marekani.
Waombolezaji waliovalia mavazi meusi waliandamana kwenye Uwanja wa Jomhouri Eslami kuelekea kwenye kitongoji ilipokuwapo ofisi ya Khamenei, aliyeuawa akiwa na umri wa miaka 86, mnamo Februari 28, na ambaye hadi leo maiti yake haijazikwa rasmi.