1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano yavunjika Sudan

19 Aprili 2023

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hasimu yaliyokuwa yaanze jioni ya Jumamme yamevunjika nchini Sudan na mashambulizi yameendelea kwenye mji mkuu, Khartoum, huku maelfu wakiyakimbia makaazi yao.

Sudan l Kämpfe im Sudan halten an l Ausgebrannte Militärfahrzeuge der RSF
Picha: Omer Erdem/AA/picture alliance

Jumatano (Aprili 19) iliamkia kwa mashambulizi mengine ya anga na miripuko katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, baada ya kushindwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani baina ya jeshi rasmi na wapiganaji wa kikosi maalum cha wanamgambo kinachoogopewa cha RSF, huku maelfu ya wakaazi wa mji huo wakijaribu kuyakimbia mapigano hayo. 

Milio ya makombora na miripuko iliendelea kusikika hadi asubuhi ikitokea yalipo makao makuu ya wizara ya  ulinzi na uwanja wa ndege, ambayo yamekuwa yakiwaniwa na pande hizo mbili tangu mapigano yalipoanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Soma zaidi: Milio ya risasi inaendelea kusikika nchini Sudan licha ya kauli ya kusitisha mapigano

Mashahidi mjini Khartoum walisema "anga zima la mji huo mkuu limejaa moshi." 

Mataifa ya kigeni, ikiwemo Marekani, yamekuwa yakishinikiza makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jeshi la vikosi vya RSF ili kuwapa nafasi raia kupata misaada na huduma muhimu. 

Kila upande waushutumu mwengine

Awali pande zote mbili zilikuwa zimeashiria kukubaliana na kusitisha mapigano kutoka saa 12:00 jioni ya Jumanne (Aprili 18), lakini muda mfupi baadaye milio ya risasi na makombora ilisikika na kila upande ulitowa taarifa ya kuushutumu mwengine kwa kutoheshimu makubaliano hayo.

Mojawapo ya nyumba ya raia zilizoharibiwa kwa mashambulizi wakati mapigano yakiendelea kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya RSF.Picha: REUTERS

Kwa upande wake, kamandi kuu ya jeshi ilisema wale inaowaita "wanamgambo waasi" wameendelea na kusababisha ghasia za hapa na pale kuzunguka makao makuu ya jeshi na uwanja wa ndege", huku taarifa ya RSF ikisema jeshi "limeendelea kuyavunja makubaliano ya kusimamisha mapigano" kwa kuzishambulia kambi zake kwenye mji mkuu, Khartoum.  

Soma zaidi: Sudan: Kuna kauli zinazokinzana juu ya usitishaji mapigano

Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba mapigano yalianza tena usiku na kisha kurejea tena alfajiri ya leo kwenye upande wa mashariki mwa mji mkuu, Khartoum, ambako wakaazi wanasema muda pekee ambao kulikuwa kimya ni baina ya saa 9:00 na 11:00 asubuhi. 

Wakaazi wa Khartoum wakimbia 

Shirika la habari la AFP linaripoti kuwashuhudia maelfu ya wakaazi wa mji huo wakikimbia makaazi yao, wengine kwa magari na wengine kwa miguu, wakiwamo wanawake na watoto.

Moshi ukitawala anga la mji mkuu wa Sudan, Khartoum, kufuatia mashambulizi ya makombora kwenye mapigano kati ya jeshi na vikosi vya RSF.Picha: Ahmed Satti/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa wakaazi hao, mitaa yao "imejaa miili na harufu za maiti."

Soma zaidi: Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan

Baadhi ya serikali za mataifa ya kigeni zimeanza mipango ya kuwahamisha maelfu ya raia wao, wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. 

Japan imesema hivi leo kwamba  wizara yake ya ulinzi imeanza matayarisho ya kuwaondoa raia wake 60 waliopo nchini Sudan, wakiwemo wafanyakazi wa ubalozi. 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, idadi ya waliokwishauawa kwenye mapigano hayo inatajwa kufikia 185 huku zaidi ya 1,800 wakijeruhiwa, ingawa Chama cha Madaktari kinaripoti kwamba idadi kamili huenda ikawa kubwa zaidi ya hapo, kwani wengi wa waliouawa na kujeruhiwa hawafikishwi hospitalini kutokana na mashambulizi.

Vyanzo: Reuters, AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW