1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha vita Gaza yakaribia kufikiwa

13 Januari 2025

Wapatanishi wa mzozo huo wamewapatia siku ya Jumatatu wawakilishi wa Israel na Hamas rasimu ya mwisho ya makubaliano ya kusitisha vita katika ukanda wa Gaza.

Mazungumzo kuhusu mpango wa usitishwaji vita huko Gaza
Wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar wakizungumza na viongozi wa nchi za kiarabu kuhusu mzozo wa GazaPicha: JONATHAN ERNST/AFP

Kulingana na taarifa kutoka kwa afisa anayefuatilia kwa karibu mazungumzo hayo, Israel na Hamas wamepokea rasimu hiyo leo Jumatatu na watatakiwa kutoa uamuzi wao ikiwa wameafiki au laa.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na wajumbe wa rais wa Marekani anayeondoka madarakani Joe Biden na wengine kutoka kwa rais mteule Donald Trump.

Hamas imeliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo kuhusu baadhi ya masuala muhimu ya  mpango huo wa kusitisha mapigano huko Gaza yamepiga hatua na kwamba kwa sasa inajitahidi kuhitimisha haraka masuala mengine yaliyosalia.

Wanasiasa wa Israel watofautiana 

Waziri wa Fedha kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Bezalel SmotrichPicha: Bezalel Smotrich/newscom/picture alliance

Kumeshuhudiwa migawanyiko upande wa Israel kufuatia makubaliano hayo huku baadhi ya wanasiasa wakidhihirisha kuyapinga makubaliano hayo.

Waziri wa Fedha kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Bezalel Smotrich ameapa kuupinga mpango wowote wa kumaliza vita vya Gaza, akisema kuwa itakuwa janga kwa usalama wa Israel na kusisitiza kuwa huu ni wakati muafaka kwa Israel kuendeleza juhudi zake za kuitokomeza kabisa Hamas.

Soma pia: Viongozi wa G20 watoa wito wa usitishwaji vita Gaza na Lebanon

Hata hivyo maafisa wakuu wa serikali ya Tel Aviv wanasema kumekuwepo maendeleo chanya katika upatikanaji wa makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza. Akizungumza mjini Jerusalem leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar amesema nchi yake inafanya kazi kwa bidii ili kufikia makubaliano ambayo yatawezesha kuachiliwa kwa mateka.

Kiongozi wa upinzani wa Israel aunga mkono

Kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Kwa upande mwingine kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid amesema anamuhakikisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu "usalama wa kisiasa" ikiwa atafikia makubaliano hayo.

"Nataka kumkumbusha tena Netanyahu - hana haja na Ben Gvir wala Bezalel Smotrich. Nampa usalama wa kisiasa kwa mkataba huu wa kuachiliwa mateka. Ofa hii ni ya wazi zaidi kuliko hapo awali. Ikiwa Netanyahu ataweza kufikia makubaliano, tutajadili kuhusu pendekezo hili la usalama ndani ya nusu saa, " alisema Lapid.

Mapema Januari, mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani yameanza tena mjini Doha ili kujaribu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo pia yatawezesha kuachiliwa kwa makumi ya mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa huko  Gaza  huku wafungwa wa Kipalestina wakiachiliwa pia huru.

Hayo yakiarifiwa, Norway itakuwa mwenyeji wa mazungumzo yatakayohudhuriwa na makumi ya nchi ili kujadili suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina. Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammed Mustafa, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini, na mjumbe wa Umoja wa Mataifa huko Mashariki ya Kati Tor Wennesland ni miongoni mwa wale watakaohudhuria.

Licha ya yote hayo, mapigano yameendelea kuripotiwa huko Gaza ambapo leo hii watu saba wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia shambulio la droni la Israel katika kitongoji cha al-Daraj.

(Vyanzo: AFP, Reuters, AP, DPA)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW