Makubaliano ya kusitisha vita yaanza Gaza
19 Januari 2025Utekelezaji huo umeanza baada ya Kundi la wanamgambo la Hamas kutangaza orodha ya majina matatu ya Waisrael watakaoachiliwa huru.
Mapema leo asubuhi jeshi la Israel liliendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza likisema, utekelezaji makubaliano hayo umecheleweshwa na Hamas, kwa kutotowa orodha ya mateka itakaowaachilia.
Soma pia: Israel itawaachilia zaidi ya wafungwa 1900 wa Kipalestina
Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alitowa taarifa kupitia televisheni,akisema jeshi linaendelea kufanya mashambulizi ndani ya Gaza.
Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alitowa maagizo ya kutotekelezwa usitishaji mapigano hadi Hamas itakapotimiza ahadi zake. Shirika la habari la AFP lilionesha video ya mamia ya watu wa Gaza wakishangilia mapema alfajiri katika mji wa Deir el-Balah,muda ambao utekelezaji huo wa kusitisha vita ulitarajiwa kuanza.
Soma pia: Mahmoud Abbas ataja kuwa tayari kuiongoza Gaza baada ya vita
Lakini muda mfupi baadae moshi mzito ulionekana umetanda Kaskazini Mashariki mwa Gaza. Mwandishi wa habari wa AFP amesema jeshi la Israel limeshambulia Kaskazini mwa Gaza. Tariban watu wanane wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa kwa mujibu wa timu ya waokoaji wa Gaza.