Makubaliano ya amani kati ya Marekani na Iran yapiga hatua
29 Mei 2026
Marekani na Iran zimefikia makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji wa mapigano na kuondoa vizuizi vya usafirishaji kupitia Mlango bahari wa Hormuz, ingawa Rais wa Marekani Donald Trump bado hajayaidhinisha makubaliano hayo huku vyombo vya habari vya serikali ya Iran vikiripoti kuwa bado hayajakamilishwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vinne vinavyofahamu suala hilo, makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza muda wa usitishaji wa mapigano kwa siku nyingine 60 na kuruhusu kurejea kwa shughuli za kawaida za usafiri katika mlango Bahari wa Hormuz wakati pande zote mbili zikiendelea kujadiliana kuhusu masuala nyeti ikiwemo mpango wa nyuklia wa Iran.
Iwapo makubaliano hayo yataidhinishwa na viongozi wa Washington na Tehran, hatua hiyo itakuwa maendeleo makubwa zaidi kuelekea kupatikana kwa amani tangu mzozo huo ulipoanza Februari 28.
Habari za uwezekano wa makubaliano hayo zimetokea baada ya mfululizo wa mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya mataifa hayo mawili.