1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya mlango bahari wa Hormuz yakaribia

Josephat Charo
6 Agosti 2026

Iran na Oman zinakaribia kukubaliana kuhusu njia mpya ya usafirishaji kupitia Mlango Bahari wa Hormuz uliozuiliwa, kulingana na maafisa mjini Tehran.

Vereinigte Arabische Emirate Chor Fakkan 2026 | Frachtschiffe nahe der Straße von Hormus
Picha: Fatima Shbair/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran alinukuliwa akisema na shirika la habari la serikali IRNA Jumatano jioni kwamba mataifa hayo mawili ya Ghuba yamekubaliana kuhusu uratibu wa kijiografia wa njia ya urambazaji kupitia ujia huo wa majini.

Iran ilisema Jumatano iko katika hatua ya mwisho ya kuandika makubaliano na Oman kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz, na Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano yanaweza kutangazwa wiki hii. Hilo linaweza kufungua tena njia muhimu ya maji, kupunguza shinikizo kwa uchumi wa dunia na kusaidia kukomesha vita.

Lakini makubaliano hayo yanawezekana kutegemea Marekani kuondoa vizuizi vyake kwenye bandari za Iran. Utawala wa Trump hapo awali umeondoa makubaliano yoyote ambayo yangeimarisha udhibiti wa Iran kuhusu mlango bahari wa Hormuz, ambayo yangekuwa hasara kubwa kwa Marekani na kuvunja kanuni za kimataifa.

Iran imesisitiza juu ya hatua fulani ya udhibiti wa mlango bahari wa Hormuz, ikisema hautarudi kuwa njia ya wazi ya kimataifa ya majini kama ilivyokuwa kabla ya vita.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema makubaliano na Oman yako katika hatua ya mwishoPicha: Sha Dati/Xinhua/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema makubaliano na Oman yako katika "hatua ya mwisho" ya uandishi wa rasimu, na kwamba taarifa ya pamoja itatolewa "ikiwa pande fulani hazitazuia mchakato huu," inaonekana akimaanisha Marekani.

Rasimu ya makubaliano imekamilika

Maafisa wawili wa kikanda waliliambia shiika la habari la The Associated Press Jumatan kwamba wajumbe wa mazungumzo wa Iran na Oman wamekamilisha rasimu ya makubaliano ya kufungua tena mlango bahari wa Hormuz na kusubiri idhini ya mwisho kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Mojtaba Khamenei. Khamenei inaaminika kuwa alijeruhiwa katika mashambulizi ya ufunguzi wa vita na hajaonekana hadharani tangu wakati huo.

Maafisa hao, ambao waliarifiwa kuhusu mazungumzo hayo, walielezea makubaliano hayo kama suluhisho la muda kwa mzozo kuhusu Hormuz. Walisema yanahusiana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran mwezi Juni ambayo yalilenga kukomesha mapigano na kufungua tena njia ya maji lakini hatimaye yalivunjika.

Maafisa hao, ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kujadili mazungumzo ya faragha, walisema makubaliano hayo yanayowezekana yatafungua njia kwa Marekani na Iran kuanza tena mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Hapo awali, walisema makubaliano hayo yanayowezekana yangeruhusu meli kuingia Ghuba ya Uajemi kupitia njia inayodhibitiwa na Iran na kutoka kupitia njia inayodhibitiwa na Oman. Maafisa hao walisema ada za huduma zitatozwa kwa kutoa usalama na kuhifadhi mazingira ya baharini.

Rasimu ya makubaliano kuhusu mlango bahari wa Hormuz yanakaribiaPicha: Khaled Ziad/AFP

Marekani imesema inapinga vikali mpango wowote ambao ungeifanya Iran kutoza ada.

Mashambulizi dhidi ya meli za kikanda yanaendelea

Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen walidai Jumatano kwamba walikuwa wamerusha makombora ya balestiki kuelekea meli ya mafuta ya Saudi Arabia kwenye Bahari ya Shamu karibu na bandari ya Saudi Arabia ya Yanbu, bila kutoa ushahidi. Hakukuwa na maoni ya haraka kutoka Saudi Arabia.

Meli iliyokuwa ikisafiri katika Ghuba ya Aden karibu na Yemen iliripoti mlipuko mkubwa uliotokea karibu, kituo cha Operesheni za Biashara za Baharini cha jeshi la Uingereza kilisema Jumatano, na kuongeza kuwa wafanyakazi walikuwa salama. Wahouthi walidai kufyatua kombora la balestiki kwenye meli nyingine ya mafuta ya Saudi Arabia.

Kuongezeka kwa kasi hivi karibuni kati ya waasi na Saudi Arabia kunatishia kufufua vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen, ambavyo viliwakutanisha Wahouthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaounga mkono serikali ya nchi hiyo.

Makubaliano ya kati ya Israel na Hezbollah yayumba

Mkataba wa usitishaji mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah ulizidi kukabiliwa na hali tete Jumatano, huku jeshi la Israeli likitoa onyo la kuwahamisha wakazi wa kijiji cha Mansouri kusini mwa Lebanon - onyo la kwanza kama hilo baada ya wiki kadhaa.

Makubaliano ya usitishaji mapigano kati Israel na Hezbollah yanayumbaPicha: IDF/GPO/SIPA/picture alliance

Baadaye, jeshi la Israel lilisema limeanza kufanya mashambulizi sahihi kusini mwa Lebanon kujibu kile ilichokielezea kama ni ukiukaji wa wazi wa usitishaji mapigano ambao kwa kiasi kikubwa umefanyika tangu Juni 20.

Kuongezeka kwa kasi kwa mapigano kulikuja wakati wapatanishi wa Lebanon na Israel walipokutana mjini Roma kwa siku ya pili kujadili utekelezaji wa makubaliano ambayo chini yake vikosi vya Israeli vinapaswa kujiondoa kutoka maeneo wanayoyamiliki kusini mwa Lebanonkwa mabadilishano na Hezbollah kupokonywa silaha.

Afisa wa wizara ya mambo ya nje alisema mazungumzo ya mjini Roma yalimalizika mapema kutokana na matukio yaliyotokea ardhini lakini yanaweza kuendelea Alhamisi. Afisa huyo, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na mchakato nyeti wa diplomasia, alisema majadiliano hayo yalikuwa na tija kubwa sana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW