Makubaliano ya Zimbabwe yaungwa mkono
12 Septemba 2008Taarifa kutoka Zimbababwe zinadokeza kwamba rais Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wataongoza kwa pamoja serikali ya mseto itakayoundwa baada ya kufikiwa makubaliano kati ya pande hizo mbili hapo jana.
Duru zilizo karibu na ujumbe uliofanikisha kufikiwa makubaliano hayo yatakayowekwa wazi rasmi jumatatu zinasema kuwa Vigogo hao wawili wa kisiasa wataiongoza kwa pamoja nchi hiyo inayokabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.Rais Mugabe ataliongoza baraza la mawaziri wakati Tsvangirai akichukua jukumu la kuongoza baraza la usalama la kitaifa ambalo linawajumuisha mawaziri 31 wa serikali.
Duru kutoka kwenye mazungumzo kuhusu suala la kugawana madaraka nchini Zimbabwe zimeeleza kuwa madaraka ya kuliongoza taifa hilo yatagawanywa sawa kwa sawa miongoni mwa vigogo hao wawili wa kisiasa.
Imeelezwa kwamba hakuna kati ya viongozi hao wawili atakayemzidi mwengine kwa mamlaka ambapo wote wawili watakuwa na majukumu ya kuajiri na kuwatimua katika nyadhifa zao mawaziri watakaounda serikali ya mseto.Aidha imebainishwa kwamba maamuzi yote yatafanywa na baraza la usalama la kitaifa lakini baraza hilo litabidi kuripoti tena kwa rais Mugabe.
Magazeti ya Afrika Kusini hii leo pia yamechapisha taarifa hizo kwamba makubaliano yaliyofikiwa yanaweka wazi kuwa viongozi hao watakuwa na nguvu sawa za uongozi wa taifa hilo.Chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini kimeitaka jumuiya ya kimataifa kuisadia Zimbabwe kutokana na kufikiwa makubaliano hayo.
Rais Thabo Mbeki ambaye amekuwa mpatanishi mkuu katika mazungumzo juu ya kugawana madaraka amesema anaweka matumani kwamba jumuiya ya kimataifa itaunga mkono juhudi zilizofikiwa.Thambo Mbeki ameongeza kusema kuwa,
"Tunatumai kwamba kila mmoja ulimwenguni ataunga mkono makubaliano yaliyofikiwa na wazimbabwe,na kutuunga mkono zaidi kwa kutusaidia.''
Hata hivyo wakati Afrika Kusini ambayo rais wake ndiye aliyesimamia mazungumzo ya upatanishi ikiwapongeza wazimbabwe juu ya kufikia makubaliano hayo ya kihistoria, tume ya Umoja wa ulaya imeupokea mwafaka huo na tahadhari ikisema kwamba inataka kusubiri nakuona makubaliano hayo hadi hiyo jumatatu yatakapowekwa wazi.Aidha Umoja wa Ulaya umesema kwamba unafikiria upya mipango yake ya kuongeza vikwazo dhidi ya Zimbabwe kufuatia makubaliano hayo ya kisiasa.
Mjumbe wa ngazi ya juu wa Ufaransa ambayo ni mwenyekiti wa Umoja huo amesema kuwa watabidi kuitathmini hali ya mambo katika siku nzima ili kufikia uamuzi.Halikadhalika suala la Zimbabwe limepangwa kujadiliwa zaidi katika kikao cha kila mwezi cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja huo waUlaya kitakachofanyika mjini Brussels siku ya jumatatu.
Kwa upande mwingine hata hivyo mkuu wa sera za nje wa umoja huo Javier Solana amesema wametiwa moyo na hatua hiyo ya kufikiwa makubaliano nchini Zimbabwe.Katika taarifa yake bwana Solana amesema ana imani kwamba maafikianao hayo yatakayotiwa saini jumatatu yataiwezesha Zimbabawe kujikwamua katika mzozo wa kiuchumi.
Mwaka huu umoja wa Ulaya wenye wanachama 27 ulipitisha vikwazo zaidi dhidi ya watawala wa Zimbabwe ikiwemo kufunga akaunti za baadhi yao na vikwazo vya usafiri.
Nchini Kenya waziri mkuu Raila Odinga ameyakaribiasha maafikiano hayo ya kisiasa nchini
Zimbabwe akitoa mwito wa kutekelezwa haraka kwa makubaliano hayo ili kumaliza mvutano wa kisiasa katika taifa hilo.Raila Odinga ambaye binafsi alikuwa katika mvutano wa kisiasa na rais Mwai Kibaki baada ya uchaguzi wa mwaka jana nchini Kenya amesema anamatumaini kwamba makubaliano hayo yataelekeza katika kupatikana amani na kuimarishwa viwango vya maisha ya wazimbabwe pamoja na haki za binadamu nchini humo.
Hata hivyo wazimbabwe wenyewe ambao maisha yao yameharibiwa kufuatia hali mbaya ya kiuchumi wameyapokea kwa wasi wasi mkubwa makubaliano hayo ya kugawana madaraka kati ya Mugabe na Tsvangirai wengi wanasema wanafurahia lakini ni mapema mno kuanza kusherehekea.