Makundi ya Haki za binaadamu yakosoa mauaji Tanzania
7 Novemba 2025
Katika taarifa ya pamoja na mashirika mengine sita yasiyo ya kiserikali leo Ijumaa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilisema kulikuwa na "matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao hawakuwa na silaha, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kulipiza kisasi dhidi ya raia, baadhi wakiwa majumbani mwao."
Taarifa hiyo imesema na hapa nanukuu "Familia zimeachwa zikiwa na kiwewe, na watoto wameshuhudia wazazi wao wakidhulumiwa." Imeongeza kuwa mamia ya watu walikamatwa, na baadhi wameendelea kuzuiliwa bila dhamana. Taarifa hiyo ilionya kwamba "kiwango cha ukiukwaji wa haki za binadamu bado hakijawekwa wazi kikamilifu", huku ikikosoa hatua ya kufungwa kwa intaneti na mipaka kwa vyombo vya habari.
Maandamano ya vurugu yalizuka kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki siku ya Uchaguzi Mkuu huku vyanzo vikisema mamia huenda waliuawa.
Katika ripoti ya awali, waangalizi wa uchaguzi kutoka Afrika walisema uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto zilizowazuia Watanzania kuchagua viongozi wanaowataka na hasa kutokana na kuzuiwa kwa baadhi ya wagombea wa upinzani, vitisho, pamoja na dalili za wizi wa kura.
Watu 98 washitakiwa kwa uhaini
Katika hatua nyingine, waendesha mashitaka nchini humo wamewafungulia kesi ya uhaini karibu watu 98, wanaodaiwa kujihusisha na maandamano hayo ya kipindi cha uchaguzi mkuu. Haya ni mashtaka ya kwanza dhidi ya watu wanaoshukiwa kushiriki maandamano.
Hati ya mashtaka dhidi yao iliyowasilishwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Dar es Salaam imesema washtakiwa "walibuni njia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 kwa madhumuni ya kuitisha ofisi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" na kusababisha uharibifu wa mali za umma.
Hata hivyo hakukuwa na ufafanuzi zaidi kuhusu mashtaka hasa dhidi yao, isipokuwa dhidi ya mshtakiwa mmoja, ambaye ni mfanyabiashara Jenifer Jovin Bilikwija, maarufu Niffer. Niffer ameshitakiwa kwa kosa la uhaini, akidaiwa kuwahamasiha wananchi kuvuruga uchaguzi na kuwahimiza kununua barakoa za kujizuia na gesi ya kutoa machozi wakati wa maandamano, dukani kwake.
Makosa ya uhaini nchini Tanzania, mara nyingi huchukuliwa kuwa nyeti kisiasa na adhabu yake huwa ni kunyongwa hadi kufa. Rais wa chama cha wanasheria nchini Tanzania, Boniface Mwabukusi, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema washitakiwa hao hawakuwakilishwa na wakili yoyote.
Maandamano hayo yalichochewa kwa kiasi kikubwa na hasira ya raia walioghadhabishwa na hatua ya wagombea wawili kutengwa kwenye uchaguzi na wanasiasa wawili wakubwa wa upinzani kuondolewa kwenye kinyang'anyiro cha urais. Miongoni mwao, ni Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashitaka ya uhaini.