Makundi ya upinzani Syria yapata msimamo mmoja
12 Januari 2014Suluhisho lolote linapaswa kujumuisha kuufikisha mwisho utawala wa rais Bashar al-Assad na kuundwa kwa serikali ya mpito iliyo na mamlaka kamili, makundi ya upinzani yamesema baada ya mkutano wao mjini Cordoba , nchini Uhispania.
Tamko hilo lilitolewa na wawakilishi 150 wa upinzani baada ya kukamilika kwa mkutano wao wa siku mbili kusini mwa Uhispania.
Utawala wa sasa hauna nafasi kwa Syria ya baadaye
Msimamo wa kundi hilo linaloelekea katika mazungumzo yaliyopangwa kuanza baadaye mwezi huu mjini Geneva ni kwamba maafisa wa sasa katika utawala wa Syria hawatakuwa na jukumu lolote katika serikali ya mpito pamoja na hali ya baadaye ya nchi hiyo, tamko hilo limeongeza.
Wawakilishi wa upinzani pia wamesema wanaamini kwamba "mkutano wa kuliokoa taifa" ni lazima utayarishwe na wawakilishi wote wa wanamapinduzi wa Syria. Pia wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhimiza kuangushwa kwa utawala wa rais Assad na wale wanaohusika na uhalifu nchini Syria wafikishwe mbele ya sheria.
Mazungumzo hayo mjini Cordoba , ambayo yamefanyika kwa faragha, yalisimamiwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Uhispania. Madrid inauangalia mkutano huo kama mchango katika ufunguzi wa awamu ya mpito nchini Syria ambayo itaelekeza katika suluhisho la kisiasa la mzozo huo.
Marekani ina matumaini
Marekani ina imani kubwa kwamba inaweza kuushawishi upinzani nchini Syria kujiunga na mazungumzo ya amani baadaye mwezi huu. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry anajitayarisha kwenda mjini Paris kukutana kesho Jumapili(12.01.2014) na mawaziri kutoka kundi la "Marafiki wa Syria" kwa matumaini ya kukamilisha taarifa za mwisho za mkutano huo.
Mkuu wa Muungano wa taifa wa Upinzani Ahmad Jarba pia atahudhuria mazungumzo hayo katika mji mkuu wa Ufaransa, na huenda akakabiliwa na mbinyo kujiunga na mazungumzo ya Geneva 2 yanayotarajiwa kuanza Januari 22.
Wakati huo huo , wakati watu 500 wameripotiwa kuwa wameuwawa katika wiki ya mapigano ya waasi , wengi wa Wasyria wamejifungia majumbani mwao jana Ijumaa (10.01.2014), wakati wengine wakitoka kutoka misikitini wakiwa na hasira wakilishutumu kundi lenye mafungamano na kundi la al-Qaeda kwa kuteka nyara mapinduzi yao.
Mapambano kati ya waasi na waasi yamegubika mapambano dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad na kuonesha madhila yanayowapata raia ambao wanajikuta katikati ya mapambano ya vita hivyo viwili.
Ghasia , ambazo ni kati ya wapiganaji kutoka makundi kadha ya Kiislamu pamoja na makundi mengine dhidi ya kundi linaloogopwa la taifa la Kiislamu na Sham ambalo linamafungamano na al-Qaeda, yamesambaa katika majimbo manne katika maeneo yanayodhibitiwa na upinzani kaskazini mwa Syria.
Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London limesema jana Ijumaa ( 10.01.2014) kuwa kiasi watu 482 wameuwawa katika mapigano tangu Januari 3. Limesema pia kuwa watu 157 walikuwa kutoka taifa la Kiislamu la Iraq na sham, 240 ni kutoka makundi yenye msimamo wa wastani na 85 walikuwa raia.
Vifo hivyo vina akisi na hata kupindukia vifo katika vita vikuu vya nchi hiyo kati ya majeshi ya serikali na waasi katika kiwango hicho.
Wakati hayo yakitokea katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa wafadhili wiki ijayo kwa ajili ya kupatikana msaada wa dharura nchini Syria, anatarajiwa kutoa tahadhari kwa jumuiya ya wafadhili kwamba mzozo wa kiutu katika taifa hilo lililotumbukia katika matatizo , unatishia kufikia hali mbaya kabisa.
Watu zaidi wauwawa
Tangu mzozo huo ulipozuka Machi mwaka 2011, zaidi ya watu 100,000 wameuwawa, wengine zaidi ya milioni nane wamelazimika kukimbia makaazi yao na zaidi ya wengine milioni mbili wameomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani, na idadi hiyo inaongezeka.
Ofisi ya Umoja wa mataifa ya kuwahudumia wakimbizi UNHCR inakadiria kuwa kiasi ya Wasyria milioni 4.1 ni wakimbizi, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watoto milioni mbili, ambao watahitaji msaada ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Mkutano huo wa kuomba msaada mjini Kuwait uliopangwa kufanyika Januari 15 mwaka huu , unafanyika kwa hisani ya Emir wa Kuwait , Sheikh Jaber Al-Ahmad Al-Jaber Al Sabah, na ameueleza kuwa ni "tukio muhimu la kuomba msaada wa kibinadamu".
Umoja wa Mataifa umekadiria mwezi uliopita kuwa mahitaji kwa Syria yanafikia kiasi ya dola bilioni 6.5 katika mwaka 2014, ikiwa ni kiwango kikubwa kuwahi kuombwa kwa ajili ya msaada wa dharura kwa nchi moja.
Mkutano wa kwanza wa kuisaidia Syria , ambao ulifanyika mwezi Januari mwaka 2013, na kufanyika pia nchini kuwait, ulifanikiwa kupata dola bilioni 1.5 za msaada wa kiutu.
Mwandishi : Sekione Kitojo /DPAE / IPS / APE
Mhariri: Sudi Mnette